Rais Samia Suluhu Hassan amesema kuwa baada ya mazishi ya Dkt. John Magufuli , kinachofuata ni utekelezaji wa ahadi zote ambazo yeye na chama chake (Chama cha Mapinduzi) waliahidi wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Rais Samia amesema hayo jana wilayani Chato mkoani Geita wakati akitoa salamu za pole kwa familia ya Dkt Magufuli na waombolezaji wengine waliofika kwenye Misa Takatifu ya mazishi ya kiongozi huyo.

Alisema kuwa Tanzania imempoteza Jemedari, lakini watendaji na wasaidizi aliokuwa akifanya nao kazi bado wapo hivyo watatekeleza yale yote aliyoahidi kwa wananchi.

Kuhusu ahadi ya kuifanya wilaya ya Chato kuwa mkoa ambayo Dkt. Magufuli alikuwa ameahidi, Rais Samia alisema kuwa anafahamu kwamba mchakato wa hilo umeanza na amewataka watendaji kuendelea nao, na kwamba wataangalia kama vigezo vimetimia.