Rais mpya wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kiapo alichokula hii leo ni tofauti na viapo vingine alivyowahi kuvifanya katika maisha yake.

Akizungumza Ikulu mkoani Dar es salaam mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema kuwa amekula kiapo akiwa na kidonda kikubwa moyoni mwake.

Amesema kuwa viapo vyote alivyokula vilikuwa vya faraja, nderemo, vifijo na bashasha, lakini kiapo alichokula leo ni cha juu zaidi na amekula akiwa na majonzi.

Amesema kiapo chake kimekuwa ni cha uchungu kwa kuwa kipindi hiki nchi imetandwa wingi jeusi na simanzi kubwa.

Samia Suluhu Hassan ameapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muumgano wa Tanzania baada ya kifo cha Dkt. John Magufuli.