Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amemuagiza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Selemani Jafo kufuatilia upotevu wa fedha katika ofisi yake na endapo atashindwa kufanya hivyo atoe taarifa asaidiwe.


Rais Samia ametoa kauli hiyo leo Machi 28, 2021 mara baada ya kupokea ripoti kutoka kwa wa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na ripoti ya TAKUKURU ya 2019/2020, Ikulu ya Chamwino Jijini Dodoma ambapo ripoti ya CAG ilionesha katika Mamlaka ya Serikali za Mitaa, alikagua hati 185 ambapo hati zinazoridhisha ni 124, hati zenye mashaka ni 53 na hati mbaya 8.

"TAMISEMI kuna upotevu sana wa fedha, Waziri uko hapa Jafo tunaomba uhangaike mara ya mwisho ukishindwa sema tukusaidie, Tamisemi wanachukua fedha nyingi serikali kuu lakini wao hawarudishi," alisema Rais Samia.

Awali akisoma ripoti yake mbele ya Rais Samia, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Charles Kichere amesema kuwa hali ya utekelezaji wa mapendekezo anayotoa kwa serikali bado hairidhishi kwani asilimia 30 pekee ya mapendekezo ndio yamefanyiwa kazi, hivyo jitihada zaidi zinahitajika ili kuimarisha na kuongeza mapato kwa kudhibiti mifumo ya ndani.

"Kwa mwaka wa fedha 2019/2020 nimetoa jumla ya hati 900 za ukaguzi ambapo nimetoa kwa Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Miradi ya Maendeleo, Mashirika Binafsi pamoja na Vyama vya Siasa, kati ya hizo hati zinazoridhisha ni 800 sawa na 89% hati zenye shaka ni 81 sawa na 9% mbaya 10 sawa na 1%", imebainisha ripoti ya CAG Charles Kichere.