Rais  wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameigiza Wizara ya Nchi, Ofis ya Rais, Fedha na Mipango kuendelea na jukumu la kutafuta fedha za miradi na kuziachia Wizara na taasisi kuingia katika mikataba.


Dk. Mwinyi ametoa ufafanuzi huo Ikulu Jijini hapa katika mkutano uliojadili Utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa kwa Mawaziri na Makatibu Wakuu wakati alipowaapisha.


Amesema kazi ya hazina ni kutafuta fedha, hivyo akaitaka Wizara hiyo kuondokana na utamaduni uliozoeleka wa kutafuta fedha za miradi  na kuingia mikataba, jambo ambalo linapswa kufanywa na Wizara au taasisi husika.


Akitoa mfano wa mradi wa ZUSP, Dk. Mwinyi alisema Wizara hiyo iliingia mkataba bila kuzishirikisha sekta zinazohusika, hivyo kuwepo na usimamizi dhaifu wakati wa utekelezaji wa mradi huo.


Akigusia changamoto ya upungufu wa wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Dk. Mwinyi alisema IT ni taaluma maalum, hivyo watumishi wanaopaswa kuajiriwa ni lazima wafanyiwe usaili na wataalamu wa fani hiyo, jambo linalohitaji kuangalia na Tume ya Ajira.


Alieleza pia kuna umuhimu kuangalia namna ya kuwalipa mishahra mizuri wataalamu hao, kwa kuzingatia kuwepo taasisi mbali mbali zenye mahitaji.