Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Fortunatus Muslimu, amesema kuwa Polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio la mgonjwa Piche Mkuja, anayedaiwa kumchoma kisu muuguzi wa kituo cha kuhudumia wagonjwa wa ukoma Nazareti, Ifakara wilayani Kilombero, Agatha John (50), lililotokea Machi 7, Mwaka huu baada ya mgojwa huyo kufika hospitalini hapo kwa ajili ya kupatiwa matibabu.

Muslimu amesema muuguzi huyo alifika katika eneo alikolazwa mgonjwa huyo ili kukagua maendeleo yake ndipo baada ya kufika karibu, mgonjwa huyo alichomoa Kisu na kumchoma muuguzi tumboni hadi utumbo ukatoka nje kisha na yeye kujichoma sehemu za tumboni kwa lengo la kutaka kujiua.

Muslimu ameendelea kusimulia kuwa baada ya tukio hilo wafanyakazi wezake walimchukua muuguzi huyo na kumpeleka katika Hospitali ya St.Francis ili kupatiwa matibabu ambapo muda mchache badae alifariki

"Hadi sasa upelelezi unaendelea kwani mara baada ya tukio muuguzi alifariki, mtuhumiwa sasa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya St. Francis chini ya ulinzi mkali wa Polisi, taarifa za awali zinaonesha mtuhumiwa ni mzima wa afya na wala hana tatizo la akili, tunachunguza kujua chanzo,” amesema RPC Muslimu.