Vilio, huzuni na machozi  vilitawala kila kona ya Jiji la Dodoma baada  ya mwili wa aliyekua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli aliyefariki Machi 17 mwaka huu kutua jijini Dodoma.


Mwili wa Dk Magufuli ulitua katika uwanja wa Ndege wa Dodoma majira ya saa 12:54 za jioni na kupokelewa na Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Wananchi wa Jiji la Dodoma ambao licha ya mwili wa Hayati Dk Magufuli kuchelewa kufika bado walizidi kujipanga barabarani bila kuchoka wakiimba nyimbo za mapambio.

Wingi wa wananchi waliojumuika kwenye barabara za jiji la Dodoma wakiimba 'Jeshi Jeshi Jeshi, Rais Rais Rais, Baba Baba Baba, Magu Magu Magu huku wengine wakilia ni uthibitisho tosha kwamba Dk Magufuli alikua kipenzi cha watanzania.

Wananchi wa Dodoma waliusindikiza mwili wa Dk Magufuli kutokea Uwanja wa Ndege kupitia mitaa ya Chako Ni Chako kuelekea Bunge hadi Ikulu Chamwino .