Kwenye mkesha wa ziara yake ya kihistoria nchini Iraq, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani Papa Francis ametoa heshima zake leo kwa wale wote wanaoteseka kutokana na miaka mingi ya machafuko, akisema atakwenda nchini humo kama "msafiri wa amani." 

Katika ujumbe wa video, Papa Francis ambaye ana umri wa miaka 84 amewapa mkono waumini wa dini nyingine, lakini pia akaangazia hasara kubwa iliyotokea kwa jamii za Kikristo nchini Iraq akisema kumekuwa na vifo vingi mno. 

Amesema ataenda Iraq kama msafiri anayetubu kwa ajili ya kuomba msamaha na maridhiano kutoka kwa Mungu baada ya miaka mingi ya vita na ugaidi. 

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki, ambaye anafanya ziara yake ya kwanza ya kigeni tangu kuzuka kwa janga la virusi vya corona barani Ulaya mwaka mmoja uliopita, atawasili Iraq kesho Ijumaa kabla ya kushiriki katika matukio mengi hadi Jumapili. 

Miongoni mwa matukio ya aina yake ya ziara hiyo ni mkutano wake wa ana kwa ana na Ayatollah Mkuu Ali Sistani, ambaye ni kiongozi mkuu mwenye mamlaka ya kidini kwa Waislamu wengi wa madhehebu ya Shia duniani.