Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis ameadhimisha Ibada ya Misa katika Kanisa Katoliki la Walkadea la Mtakatifu Joseph mjini Baghdad, Iraq. 

Papa Francis anakuwa kingozi wa kwanza wa Kanisa Katoliki kuongoza Misa kwa kutumia liturjia ya Ibada ya Kanisa Katoliki la Mashariki. 

Papa Francis, mwenye umri wa miaka 84, amewaambia waumini kuwa sio matajiri na wenye nguvu ambao wamebarikiwa, ''bali wale wanaowahurumia ndugu zao.'' 

Mkuu wa Kanisa Katoliki la Walkadea, Kadinali Louis Raphaeli I Sako, ameiita zira ya Papa Francis kama ''iliyopokelewa kwa furaha na Kanisa lote.'' 

Mapema jana, Papa Francis alishiriki katika mkutano wa kihistoria na kiongozi wa Waislamu wa madhebu ya Shia, Ayatollah Ali al-Sistani kwenye mji mtakatifu wa Najaf. 

Pia alilizuru eneo linaloaminika kuwa sehemu ya kuzaliwa Abrahamu. Leo Papa Francis anatarajiwa kuizuru Mosul ambayo ilikuwa ngome kuu ya kundi linalojiita Dola la Kiislamu, IS.