Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani Papa Francis anayeendelea na ziara yake ya kihistoria nchini Iraq amewatolea wito viongozi na watu wa nchi hiyo kuepuka vurugu na mivutano ya kidini. 

Papa Francis anafanya ziara ya siku nne nchini Iraq ambayo ni ya kwanza kufanywa na kiongozi wa Kanisa Katoliki kwenye taifa hilo la mashariki ya kati. 

Usalama umeimarishwa kwa ajili ya kumlinda kiongozi huyo wa kanisa katoliki baada yakutokea mashambulio ya roketi na yale ya kujitoa muhanga katika siku za hivi karibuni nchini humo. 

Wakati huo huo hatua za kiafya zinazingatiwa zaidi kutokana na hali ya maambukizi ya virusi vya corona yanayoongezeka nchini Iraq. 

Baba mtakatifu atakutana na kiongozi wa madhehebu ya Shia nchini Iraq, Ayatollah Ali Sistani pamoja na pia atazuru miji minne ukiwemo mji wa Mosul ambako makanisa na turathi nyingine zimeharibiwa na wanamgambo wa itikadi kali.