Kwa mara nyingine, Pakistan imeipiga marufuku kampuni ya mtandao wa kijamii ya Tiktok kwa madai ya kukiuka maadili ya kimaudhui, lakini mratibu wa vyombo vya habari nchini humo hakusema wazi ikiwa marufuku hiyo ni ya muda tu au ni ya kudumu. 

Korti kuu ya Peshawar ilisema baadhi ya vidio zilizopakiwa kwenye jukwaa la Tiktok hazikubaliki kwa jamii ya Pakistani. 

Hii ni mara ya pili kwa Pakistan kupiga marufuku kampuni hiyo kutoka China, mara ya kwanza ikiwa Oktoba mwaka jana, ambapo mtandao wake ulifungiwa kwa siku chache kutokana na kuchapisha video za uasherati. 

Wakati huo Tiktok iliihakikishia serikali ya Pakistan kuwa itakuwa makini kuzingatia masharti ya utamaduni wa nchi hiyo. 

Mawakili wawili walioomba marufuku hii mpya, wameihimiza korti kuuzui mtandao wa Tiktok hadi pale itakapoheshimu maagizo yaliyotolewa na mratibu wa vyombo vya habari nchini Pakistan.