Rais wa Zanzibar, Hussein Mwinyi leo Machi Mosi amemtangaza kada wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Sharif kuwa Makamu wa kwanza wa Rais akimrithi marehemu Maalim Seif Sharif Hamad.


Hatua hiyo imekuja baada ya chama cha ACT Wazalendo kukamilisha mchakato wa kupendekeza jina la atakayerithi nafasi hiyo katika kikao kilichoketi mwishoni m wa wiki iliyopita.


Taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi wa Zanzibar, Mhandisi Zena Said imesema Rais Mwinyi amezingatia kifungu cha 9(3) cha Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984.


Kifungu hicho kinasema, ‘Muundo wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar utakuwa wa Umoja wa Kitaifa na utendaji wa kazi zake utafanywa katika utaratibu utakaohakikisha kuendelezwa kwa umoja nchini na kutimiza lengo la kufikia demokrasia.’


Taarifa hiyo pia imesema Rais wa Zanzibar, Dk Mwinyi pia amepewa uwezo chini ya kifungu Namba 39(3) cha Katiba ya Zanzibar


Imesema uteuzi huo unaanza leo Machi Mosi na sherehe za kumwapisha Masoud zitafanyika kesho Machi 2 katika ukumbi wa Ikulu ya Zanzibar.