Naibu Waziri TAMISEMI Mhe. David Silinde amefanya ziara ya siku moja wilayani Busega. Katika ziara hiyo ameweza kukagua na kuridhishwa na ujenzi wa miradi ya elimu inayotekelezwa. Ameyasema hayo alipotembelea Shule ya Sekondari Antony Mtaka kukagua miradi ya ujenzi wa miundombinu katika shule hiyo.

Akiwa katika Shule hiyo, Silinde amekagua mradi wa ujenzi wa bwalo, maabara, vyumba viwili vya madarasa na ujenzi wa vyoo, ambapo Serikali imetoa jumla ya TZS Milioni 196.6 kwaajili ya ujenzi wa miradi katika Shule hiyo.

Mhe. Silinde ametaka kuwepo kwa usimamizi bora wa fedha zinazotolewa na Serikali ili kukamilisha miradi kama azma ya kufanikisha lengo la Serikali. “Nimeridhishwa na hali ya ujenzi wa miundombinu iliyofanyika katika Shule hii, sababu nimeona thamani ya fedha, nimeona matumizi bora ya fedha za serikali na pia nimeona ubora wa majengo, hii ni kwasababu ya usimamizi bora uliopo hapa” aliongeza Silinde.

Awali, akisoma taarifa fupi ya Shule hiyo, Mkuu wa Shule ya Sekondari Antony Mtaka Bw. Joseph Kazimoto amesema ukamilikaji wa ujenzi wa miradi hiyo kutasaidia kuongeza ufanisi katika ufundishaji, kupunguza uhaba wa vyumba vya madarasa na kupunguza utoro kwa wanafunzi. Hata hivyo Bw. Kazimoto ametaja changamoto za miundombinu muhimu zinazoikabili Shule hiyo ikiwemo upungufu wa madarasa, jengo la utawala na maktaba.

Kwa upande mwingine, Mhe. Silinde ameongea na Wanafunzi wa Shule hiyo na kuwataka kuweka bidii katika masomo, kwani Taifa linawategemea pia amewaeleza kwamba Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli inaendelea kutatua changamoto zote zinazoikabili sekta ya elimu nchini, ili kuweka mazingira bora kwenye Shule na Taasisi za elimu nchini.

Ziara ya Mhe. Silinde wilayani Busega ilihitimishwa katika Shule mpya ya Venance Mabeyo, inayojengwa kijiji cha Nyamikoma, kata ya Kabita. Akiwa katika Shule hiyo, amekagua na kuridhishwa na ujenzi unaoendelea na kutoa maagizo ya taratibu za awali kufanyika kwa haraka ikiwemo kuisajili Shule hiyo ili ianze rasmi kutumika.