Rais Emmerson Mnangagwa wa Zimbabwe amesema leo ni siku kubwa sana kwa Taifa la Tanzania, lakini pia ni siku kubwa kwa Zimbabwe kwani wananchi wake wanaomboleza na Watanzania kifo cha aliyekuwa Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli.

Akizungumza katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma wakati wa shughuli ya kitaifa ya kuaga mwili wa Dkt Magufuli, Rais Mnangagwa ametoa pole kwa Rais Samia Suluhu Hassan na mke wa Dkt. Magufuli Mama Janeth Magufuli, kwa kumpoteza kiongozi huyo ambaye ni ndugu wa Waafrika na wananchi wote wa Zimbabwe.

Amesema Wananchi wa Zimbabwe wanaendelea kuwaombea Watanzania katika kipindi hiki kigumu.

Rais Mnangagwa amesema Dkt. Magufuli atakumbukwa kuwa ni Mwanaume wa vitendo, aliyesaidia kulijengea heshima Taifa lake, kwani ameharakisha maendeleo ya Taifa hilo.

Rais huyo wa Zimbabwe amesema maendelea ya kiuchumi nchini Tanzania yaliyopatikana chini ya uongozi wa Dkt. Magufuli yalihamasisha wananchi wa Zimbabwe kuamini kuwa nao wanaweza kujipatia maendeleo bila kutegemea misaada kutoka nje.

Amesema Dkt. Magufuli atakumbukwa kwa jinsi alivyosimama kidete kuhakikisha kuwa vikwazo vya kimataifa ilivyowekewa Zimbabwe vinaondolewa.

Aidha amesema Dkt. Magufuli alikuwa kiongozi wa kwanza kuipatia msaada wa chakula nchi yake baada ya kukumbwa na kimbunga Idai, kimbunga kikali kilicholeta maafa makubwa Zimbabwe.

Rais Mnangagwa amesema Zimbabwe itaendelea kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan na Watanzania wote kutimiza ndoto zilizoanzishwa na Dkt. Magufuli.