Marekani imewawekea vikwazo maafisa saba waandamizi wa Urusi baada ya kuhusishwa na tukio la kumtilia sumu mkosoaji wa serikali Alexei Navalny.

Wakizungumza na waandishi wa habari, maafisa wakuu wa Ikulu ya Marekani wamesema vikwazo hivyo viliwekwa kwa ushirikiano na Umoja wa Ulaya, na kutaka Navalny kuachiliwa huru. 

Hatua ya kuwekewa vikwazo dhidi ya maafisa saba waandamizi wa Urusi akiwemo mkuu wa idara ya ujasusi, pamoja na mashirika 14 kunaashiria msimamo wa Rais Joe Biden tofauti na mtangulizi wake Donald Trump aliyeonekana kusita kuikabili Urusi.

Navalny mwenye umri wa miaka 44, aliugua alipokuwa katika safari ya ndege mnamo mwezi Agosti. Alisafirishwa hadi Ujerumani ambapo madaktari walithibitisha kuwa alitiliwa sumu iliyoshambulia mfumo wake wa neva. Urusi imekanusha kuhusika kwake na tukio hilo.