Serikali ya Marekani inatarajia leo Jumatatu kutoa tamko kuhusu Saudi Arabia kufuatia ripoti ya kijasusi ya Marekani kusema kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa taifa hilo Mohammed Bin Salman aliamuru mauaji ya muandishi habari Jamal Khashoggi.

Rais wa Marekani Joe Biden, mwishoni mwa wiki iliyopita, alisema atatangaza Jumatatu wiki hii hatua watakayochukua kwa Saudi Arabia.

Utawala wa Biden umekosolewa hasa katika ripoti ya gazeti la Washington Post iliyosema Biden angeonesha nguvu zake kwa Mohammed Bin Salman ambaye hakuwekewa vikwazo vya aina yoyote licha ya kutajwa kuhusika na mauaji ya Khashoggi.

Wiki iliyopita Saudi Arabia ilifutilia mbali madai ya kumhusisha Mohammed Bin Salman Bin Salman na kifo cha Khashoggi yalitolewa katika ripoti ya kijasusi iliyotolewa na Marekani ikifichua kuwa Mwana mfalme huyo aliidhinisha mauaji ya mwandishi habari Jamal Khashoggi mwaka 2018.

Hapo kabla Saudi Arabia ilisema mauaji ya Khashoggi kwenye ubalozi mdogo wa Saudi Arabia nchini Uturuki yalifanywa katika operesheni ya kihalifu na kukanusha kuhusika kwa mwanamfalme Salman.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken alisema Washington inalenga kuchukua mwelekeo mpya wa kisera lakini siyo kuvuruga mahusiano yake na Saudi Arabia ambayo ni mshirika wa karibu wa usalama kwenye eneo la Mashariki ya Kati.

Mwandishi huyo aliyekuwa na umri wa miaka 59 wakati wa mauaji yake, aliambiwa na balozi wa Saudia afike katika ubalozi wa taifa hilo mjini Istanbul, ili kupata nyaraka kadhaa alizohitaji ili aweze kufunga ndoa na mpenzi wake raia wa Uturuki, Hatice Cengiz.