Marekani inapanga kufanya mazoezi ya siri ya kijeshi kwa lengo la kukabiliana na China na Urusi kufuatia kuongezeka uhasama na nchi hizo mbili.

Kwa mujibu wa mtandao wa CNN, mazoezi hayo ya kijeshi yatasimamiwa na Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Marekani, Mark Milley, na kufuatiliwa kwa karibu na Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin. 

Imedokezwa kuwa mazoezi hayo yatajumuisha majeshi yote ya Marekani duniani na yatafanyika miezi kadhaa tu baada ya Joe Biden kuwa rais wa Marekani.

Hivi karibuni Urusi ilimuita nyumbani balozi wake mjini Washington kwa kile kilichotajwa kuwa ni kuchunguza uhusiano wa siku zijazo na Washington baada ya Rais wa Marekani, Joe Biden kumtaja mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin kuwa ni "muuaji".

Aidha Uhusiano kati ya Marekani na China umekuwa mbaya kwa miaka mingi na inaonekana bado uhusiano huo unaendelea kuwa mbaya.

Hali kadhalika Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Anthony Blinken hivi karibuni alitoa wito kwa washirika wa muungano wa kijeshi wa NATO kushirikiana katika kukabiliana na kile alichodai ni tishio la China.

-Parstoday