Mangula: Rais Samia Atakamilisha Kazi Zote Zilizobaki
Makamu mwenyekiti wa CCM, Philip Mangula amesema aliyekuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan alitembea pamoja nchi nzima na aliyekuwa rais wa Taifa hilo, Hayati John Magufuli kunadi Ilani ya CCM yenye kurasa 303 hivyo kiongozi mkuu huyo atakamilisha kazi.
Mangula ameeleza hayo leo Jumatatu Machi 22, 2021 katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma wakati wa kuaga mwili wa Magufuli.
“Kuna simanzi kubwa, majonzi na masikitiko makubwa halafu kuna hofu na wasiwasi kwamba rais tuliyemzoea ameondoka hatupo naye sasa itakuwaje?”
“Nataka tu nikumbushe kwamba Rais Magufuli wakati huo na Samia Suluhu Hassan ndiyo waliopita nchi nzima kueleza shabaha na makusudio ya chama chetu ya mambo ya kufanya kwa miaka mitano ijayo,” amesema Mangula.
Amesema wawili hao walianza miaka mitano iliyopita kwa kupita nchi nzima na Ilani wakinadi kazi na wakarudi mwaka 2020 kuomba ridhaa kwa wananchi kukamilisha kipindi cha pili.
“Walipita nchi nzima kuwaambia tuliyopanga kufanya yajayo wananchi walikubali kwa asilimia 84.7 na baada ya kukubali Serikali ilipanga namna ya kutekeleza zile ahadi baada ya mpango wa maendeleo wa Serikali utakwenda kwenye bunge, ambalo linakutana kujadili mpango wa maendeleo wa utekelezaji wa zile ahadi zote. Msikate tamaa kazi itafanyika,” amesema Mangula.