Malkia Elizabeth wa II wa Uingereza amejibu madai ya ubaguzi kutoka kwa mjukuu wake Mwanamfalme Harry na mkewe Meghan, akielezea wasiwasi mkubwa na kuonyesha huruma kuhusu matatizo wanayopitia ya maisha ya kifalme. 

Taarifa kutoka Kasri la Buckingham imesema familia nzima imehuzunishwa na habari za jinsi miaka kadhaa iliyopita ilivyokuwa migumu sana kwa Harry na Meghan. 

Imesema masuala yaliyoibuliwa, na hasa kuhusu ubaguzi, ni ya kutia wasiwasi. Malkia amesema mambo hayo yamechukuliwa kwa uzito mkubwa na yatashughulikiwa na familia hiyo kwa njia ya faragha. 

Kasri la Buckingham limekumbwa na shinikizo la kutaka lizungumzie madai yaliyotolewa kwenye mahojiano ya kipindi cha televisheni cha Oprah Winfrey kilichorushwa kwa mara ya kwanza Jumapili iliyopita, ambayo yalizusha mgogoro ambao haujaonekana tangu nyakati za mamake Harry, Dianna katika miaka ya 1990.