Nchi jirani za Myanmar zimeushinikiza utawala wa kijeshi wa Myanmar kumuachilia huru kiongozi aliyepinduliwa Aung San Suu Kyi, na ukomeshe kile ambacho Singapore imetaja kuwa matumizi mabaya ya nguvu kali dhidi ya wapinzani wa mapinduzi yao ya Februari mosi, na badala yake ushirikiane kutafuta suluhisho la utata ulioko.

Wito kutoka nchi wanachama wa muungano wa nchi za kusini mashariki mwa Asia (ASEAN) umejiri mnamo wakati polisi wa Myanmar kwa mara nyingine wamefyatua risasi na gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji, wanaopinga utawala wa kijeshi. 

Walioshuhudia wamesema watu kadhaa walijeruhiwa.Mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa ASEAN wamefanya mazungumzo na wawakilishi wa kijeshi kwa njia ya video, siku mbili baada ya machafuko na umwagaji mbaya wa damu kutokea tangu jeshi lilipoipindua serikali iliyochaguliwa ya Suu Kyi.

Watu wasiopungua 21 wameuawa nchini Myanmar tangu mapinduzi hayo.Waziri wa mambo ya nje wa Indonesia ameihimiza Myanmar kufungua milango kwa mataifa ya ASEAN kuingilia kati ili kusuluhisha mvutano unaozidi kuongezeka.