Korea Kaskazini imefyatua makombora yake ya kwanza ya masafa marefu tangu Rais wa Marekani Joe Biden alipoingia madarakani, wakati ikitanua uwezo wake wa kijeshi na kuongeza mbinyo kwa Marekani huku mazungumzo ya nyuklia yakiwa yamekwama. 

Waziri Mkuu wa Japan Yoshihide Suga amesema makombora hayo yanatishia amani na usalama wa Japan na kanda nzima, na kuwa Japan itashirikiana kwa karibu na Marekani na Korea Kusini kuhusu vitendo vya majaribio ya makombora ya Korea Kaskazini. 

Waziri wa Mambo ya Kigeni ya Korea Kusini Chung Eui-yong, baada ya kuzungumza na mwenzake wa Urusi, mjini Seoul, ameelezea wasiwasi mkubwa kuhusu majaribio hayo ya makombora na kuitaka Korea Kaskazini kuheshimu ahadi yake ya amani. 

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov ametoa wito wa kuanza tena haraka marungumzo ya kuutatua mkwamo huo na Korea Kaskazini.