Ndugu Watanzania wenzangu, Bwana Yesu asifiwe sana. Ni jambo la kumshukuru Mungu kwa sababu ya uzima tulio nao. Vilevile tumeagizwa katika neno lake kwamba “shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu.” (1 Thes. 5:18).

Ama kwa hakika kifo cha rais wetu Dr. John Pombe Joseph Magufuli ni pigo kubwa kwa nchi yetu. Kwa Mtanzania yoyote, mpenda maendeleo ya nchi, ni lazima kwa namna moja au nyingine ameguswa na msiba huu mkubwa kwa taifa letu. Ni kweli kwamba Hayati Magufuli alifanya mambo mengi mazuri kwa Watanzania ambayo si rahisi kuanza kuyataja moja moja na kuyamaliza; . Haya yote kwa sasa hatuna haja ya kuyajadili.

Niungane na watumishi wengine wote ambao wametoa pole kwa familia ya Hayati Dr. Magufuli, kwa Mh. Samia Suluhu Hassani, na kwa watanzania wengine wote ujumla wake. Tuendelee kumwomba Mungu atutie nguvu katika kipindi hiki kigumu cha msiba.

Hoja yangu kwa sasa ni kwamba kumeibuka kundi la watu mtandaoni wakijirekodi huku wengine wakimtukana Mungu .Huku wengine, ama kwa kutokujua au kwa kujua wakifurahia kana kwamba jambo hili ni la kufurahisha katika jamii zetu. Hapa unajiuliza, “huyu mtu amepata wapi nguvu za kujirekodi, ilhali ana maumivu?

Ieleweke kwamba, kila mtu ana thamani yake.  Kila mtu ana thamani sawa mbele za Mungu, na kwa hiyo tusitafute kiki

Tunahitaji kujua mambo yafuatayo:-

1.      Mungu huamua kumchukua yeyote anayemtaka, kwa wakati ufaao kwake, na kwa jinsi apendavyo yeye, na bado anabaki kuwa Mungu. Kwa hiyo, hakuna mtu ambaye anaweza akaropoka mbele za Mungu na kuanza kumtukana . Tunapaswa kujua kwamba Wakristo kifo ni mwanzo wa maisha mengine. Tunasoma hivi, “Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana.” (Warumi 14:8)

2.      Misiba ya Kikristo si ya kulia, bali ni ya kutafakari mapenzi ya Mungu. Kila tukio; jema au baya lina mapenzi ya Mungu ndani yake. Kuna wakati Mungu huamua, kama apendavyo yeye kumchukua mja wake kwa kadri apendavyo. Hata hivyo ikumbukwe kwamba Mungu katika mapenzi yake huweza pia kuruhusu visababishi vingine (second cause) kurahisisha kusudio lake. Hata hivyo, neno la Mungu linasema hivi, “Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. 14Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. (1 Thes. 4:13-14)

3.      Kumlalamikia Mungu  ni kitendo cha kukufuru; kwa maana ya kwamba wewe hukubaliani na Mungu, ambaye vitu vyote viko chini yake, anayetawala majira na nyakati, ambako kwake hakuna kubadilika!

4.      Kitendo cha kukufuru kinaweza kusababisha hasira ya Mungu kushuka kwenye taifa letu .Ama kwa hakika naweza kusema hivi, mazingira ya huzuni ni mazingira hatari sana, ambayo Shetani anaweza kuyatumia vizuri sana kukamilisha ajenda yake na inaweza kupelekea kushindwa kumtegemea Mungu katika kipindi hiki kigumu cha msiba mkubwa kwa taifa.

Wito wangu;

1.      Napenda kuwakanya wasanii wanaotumia mwanya huu kutafuta kiki waache mara moja. Ni lazima kila mmoja aweza kutawala huzuni .

2.      Katika kipindi hiki cha msiba, sisi kama taifa hebu tutumie muda mwingi:-

a)      Kutafakari ukuu wa Mungu na mapenzi yake. Na pengine kumuuliza Mungu kwa nini jambo hili limetokea sasa, yaani mtamani kuyajua mapenzi ya Mungu katika Bwana.

b)      Kama kuna watu ambao kwa namna moja au nyingine hawakuwa sawa, basi ni kipindi cha kusameheana, na kuanzisha mahusiano mapya

c)      Kumwomba Mungu kwa ajili ya kiongozi wetu mpya, ambaye anaongoza watu walewale ambao kiongozi aliyeondoka alikuwa akiwaongoza.

d)     Tukumbuke kauli ya Hayati Magufuli, “kufa tutakufa tu.”

Haya ni mawazo yangu binafsi, wala siwakilishi kanisa la Mungu,

Mungu ibariki Tanzania katika kipindi hiki kigumu cha msiba wa kitaifa

Mch. Daniel John Seni

Shekinah Presbyterian Church in Tanzania

Madale/Mivumoni-Dar es saalam

+255 769 080 629