Na Debora Sanja,BUNGE
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Selemani Kakoso imeridhishwa na ujenzi wa mradi wa treni ya mwendo kasi(SGR) na kwamba mambo mengi ambayo Kamati hiyo imekuwa ikiishauri Serikali yamefanyiwa kazi.

Akizungumza mara baada ya kukagua ujenzi wa reli hiyo ya kisasa katika kipande cha Dodoma hadi Morogoro, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Selemani Kakoso alisema kazi iliyofayika hadi sasa ni kubwa ni imefanywa kwa ufanisi.

“Kamati inaipongeza Serikali kwa hatua hii ya ujenzi inayoendelea, kuna maendeleo makubwa sana yanafanyika, hata yale mambo tuliyokuwa tukishauri Bungeni yamefanyiwa kazi,” alisema.

Mheshimia Kakoso alisema baadhi ya mambo waliyoyashauri ni pamoja na ulipwaji wa fidia kwa wananchi  huku akisisitiza Serikali kumaliza kulipa fidia hizo kwa maeneo machache yaliyosalia.

Aidha, alipongeza namna ambavyo wazawa wamepewa kipaumbele  cha ajira ambapo uwiano ni asilimia 80 kwa wazawa na asilimia 20 kwa wageni.

Kwa upande wake Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Dkt. Leonard Chamuriho alisema ujenzi wa Reli ya SGR kutoka Dar es salaam hadi Morogoro umekamilika kwa zaidi ya asilimia 90 huku ile ya kutoka Morogoro hadi Makutupora Dodoma imefikia asilimia 50.

Alisema wanatarajia  kupata kupata treni ya Umeme Juni mwaka huu na kwamba wataifanyia majaribio katika kipande cha Morogoro na Dar es Salaam na kipande cha  kutoka Morogoro hadi Makutupora Dodoma itaanza kufanya kazi baada ya kukamilika

Alisema katika Afrika kwa ujumla reli ya SGR inayojengwa nchini Tanzania ndiyo reli bora na inaweza kuhimili mzigo mzito wa  tani 35.

Kamati ya Miundombniu ipo katika ziara ya kutembelea miradi mbalimbali katika mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro.