Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo ,Mifugo na Maji imepongeza jitihada za wizara ya kilimo kuzalisha mbegu bora za mazao ya kilimo kupitia Wakala wa Taifa wa Mbegu (ASA)

Hayo yameelezwa jana Morogoro (15.03.2021) na Mwenyekiti wa Kamati hiyo Dkt. Christine Ishengoma alipoongoza wajumbe kukagua utendaji kazi wa Wakala wa Mbegu nchini (ASA) pamoja na  ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu (TOSCI).

"Tunapongeza wakala wa mbegu ASA kwa kushika nafasi ya tano kati ya makampuni 42 yanayozalisha mbegu  ambapo kwa mwaka 2019/20 ilizalisha tani 1,750 za mazao mbalimbali" alisema Dkt.Ishengoma.

Naye Mtendaji Mkuu wa ASA Dkt. Sophia Kashenge akiwasilisha taarifa kwa kamati ya kudumu ya Bunge alisema kwa kushirikiana na makampuni manane wamefanikiwa kuzalisha mbegu kwenye mashamba ya serikali toka tani 3,450 mwaka 2016/17 hadi tani 5,634 mwaka 2019/20.

Dkt.Kashenge aliongeza kusema katika kipindi cha miaka minne iliyopita wakala umefanikiwakuzalisha miche 342,000 ya michikichi ambapo miche 10,200 tayari imegawiwa bure kwa wakulima kwenye wilaya nne za Mkoa wa Kigoma kama ilivyoagizwa na Waziri Mkuu.

Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Prof.Adolf Mkenda alisema ili kuhakikisha nchi inafikia utoshelevu wa uzalishaji mbegu za mazao ya kilimo atazikutanisha taasisi za ASA,TOSCI na TARI ili kujadili na kuweka mkakati wa pamoja wa kitaalam kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora nyingi.

Prof. Mkenda aliwashukuru wabunge kwa kutembelea taasisi hizo zenye kazi kubwa ya kuhakikisha nchi inajitosheleza kwa uzalishaji mbegu na kuwa katika bajeti ijayo 2021/22 wizara itaomba Bunge kupitisha makadirio ya bajeti ili sekta ya mbegu ipate fedha za kutosha.

Takwimu zinaonesha katika kipindi cha miaka minne upatikanaji wa mbegu umeongezeka kutoka tani 36,614 mwaka 2015/16 hadi tani 76,725 mwaka 2019/20 huku uzalishaji wa ndani wa mbegu bora umeongezeka kutoka tani 20,604 mwaka 2015/16 hadi tani 69,173 mwaka 2019/20.