Na Debora Sanja, Bunge
Kamati ya Bunge ya Miundombinu imeitaka Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuweka msukumo wa kudai madeni ambayo Shirika la Mawasiliano (TTCL) na Shirika la Posta linawadai wateja wake.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mheshimiwa Moshi Kakoso wakati Kamati ilipotembelea ofisi za TTCL Jijini Dar es Salaam.

Alisema madeni yote sugu yakianza kulipwa yatasaidia mashirika hayo kufanya kazi kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kujiendesha kibiashara.

“Haya madeni ambayo TTCL na Shirika la Posta wanawadai wateja wao yakianza kulipwa yataleta manufaa makubwa kwa mashirika haya kwa kuwa yataweza kujiendesha kibiashara,” alisema.

Aidha, aliipongeza Serikali kwa kulisaidia Shirika la Posta kwa kulipunguzia changamoto mbalimbali ikiwemo kuwaondolea baadhi ya madeni ili liweze kujiendeleza.

Aliitaka pia Serikali  kuangalia uwezekano wa kuwapatia magari Shirika hilo la Posta ili liweze kusimama vizuri.

Mheshimiwa Kakoso pia alimpongeza Waziri wa Mawasiliano na Teknojia ya Habari Mheshimiwa Faustine Ndugulile kwa kazi nzuri aliyoifanya ya kusimamia sekta ya mawasiliano ndani ya kipindi kifupi.

“Natoa pongezi sana kwa kazi nzuri, endelea kuzisimamia taasisi zako vizuri na kazi yako itaonekana, ” alisema.

Alisema Kamati ipo tayari kushirikiana na Wizara yake na kwamba kama kuna kikwazo chochote kinachohitaji mabadiliko ya sheria wasisite kupeleka mapendekezo Bungeni.

Kwa upande wake Mheshimiwa Ndugulile aliishukuru Kamati kwa ziara hiyo na kuahidi kushirikiana kwa karibu ikiwemo kuyafanyia kazi maelekezo yote ambayo Kamati imeyatoa.

Kamati ya Miundombini mbali na kutembelea Ofisi za TTCL na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) na kupokea taarifa za utekelezaji wa majukumu yao pia ilipokea taarifa ya Shirika la Posta na Mfuko wa Mawasiliano kwa wote (UCSAF)