Rais wa Marekani Joe Biden ameiongoza dunia katika kuukosoa umwagikaji damu unaoendelea nchini Myanmar unaodaiwa kufanywa na jeshi na uliosababisha vifo vya watu 100 juma lililopita. 

Maziko ya baadhi ya waliofariki yamefanyika leo Jumatatu. Biden amesema kile kinachoendelea Myanmar ni ukatili mkubwa usiohitajika. 

Wanajeshi pamoja na polisi wanadaiwa kuwashambulia waandamanaji wanaopinga utawala wa kijeshi na wanaotaka utawala wa kiraia urejeshwe na pia kuachiwa huru kwa kiongozi aliyepinduliwa madarakani Aung San Suu Kyi. 

Umoja wa Mataifa umesema watu wengine 107 wakiwemo watoto waliuwawa siku ya Jumamosi wakati utawala wa kijeshi ukiwa katika gwaride la linaloadhimishwa kila mwaka kuonyesha uwezo wa jeshi hilo. 

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell amesema siku ya hafla hiyo iligubikwa na maafa ya kutisha na aibu kubwa. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litakutana siku ya Jumatano wiki hii kuijadili Myanmar.