Jiji la Minneapolis katika jimbo la Minnesota nchini Marekani limefikia makubaliano ya fidia na familia ya George Floyd, mwanamme mweusi aliyekufa akiwa mikononi mwa polisi mzungu mwezi Mei mwaka jana. 

Mawakili wa familia hiyo wamesema jiji litailipa dola milioni 27, ambazo ni nyingi zaidi kuwahi kutolewa katika historia ya Marekani kama fidia kwa kifo kilichotokea kwa njia za kihalifu. 

Polisi anayetuhumiwa kumuua Floyd, Derek Chauvin anakabiliwa na mashtaka ya kuuwa bila kupanga, ambayo yalinaswa katika mkanda wa vidio yakidhihirisha uonevu wa kibaguzi uliokita mizizi nchini Marekani. 

Wakili wa familia ya Floyd, Ben Crump amesema ukweli kwamba fidia kubwa zaidi kwa kifo kilichosababishwa na uhalifu imetolewa kwa maisha ya mtu mweusi, ni ishara yenye nguvu inayotuma ujumbe kwamba maisha ya mtu mweusi yana thamani nchini Marekani.