Idadi ya watu waliofariki kutokana na mfululizo wa miripuko katika kambi ya jeshi katika Jamhuri ya Guinea ya Ikweta imeongezeka na kufikia 98. 

Wizara ya afya nchini humo imesema hayo jana baada ya watu waliojitolea kuendeleza juhudi ya kutafuta miili chini ya vifusi.

Katika ujumbe kupitia ukurasa wa Twitter, wizara hiyo imesema kuwa majeruhi 299 bado wako hospitalini wanapoendelea kupata matibabu. 

Wizara hiyo imeendelea kusema kuwa imetayarisha kundi la wataalamu wa afya ya kiakili inayowajumuisha madaktari wa matatizo ya kiakili, wanasaikolojia na wauguzi kuwahudumia waathiriwa wa mkasa huo ikisema kuwa uharibifu sio tu wa mwili lakini pia wa kiakili. 

Rais wa nchi hiyo Teodoro Obiang Nguema, amesema kuwa ajali hiyo ilisababishwa na uzembe katika kushughulikia baruti na kwamba miripuko hiyo iliharibu karibu nyumba na majengo yote mjini Bata ulio na idadi ya watu zaidi ya 250,000.