Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kuwa karibu ya watu bilioni 4 duniani kote, wametazama kupitia vyombo vya habari zoezi la kuagwa kwa mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli, ambalo kitaifa lilifanyika jana Jijini Dodoma.

Kauli hiyo ameitoa leo Machi 23, 2021, visiwani Zanzibar, wakati akivishukuru vyombo vya habari mbalimbali ambavyo vimejitoa kurusha mubashara shughuli zote za kuaga mwili wa Hayati Dkt. Magufuli.

"Nashukuru vyombo vya habari na kwa kweli mmekua nasi tangu siku ya kwanza hata tukio hili mnalirusha duniani kote, mpaka jana jioni tunazo taarifa waliofuatilia tukio la kuaga mwili wa Hayati Dkt. Magufuli, kitaifa jana Dodoma ni watu karibu bilioni 4, walikuwa wanafuatilia tukio la kuaga kwa mpendwa wetu," amesema Waziri Mkuu Majaliwa.

Shughuli ya Kitaifa ya kuaga mwili wa Magufuli ilifanyika jana katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma ikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Mwili wa Magufuli leo unaagwa katika uwanja wa Amaan Zanzibar na utalala katika Ikulu ya Zanzibar.