Na Faraja Mpina – WMTH, Zanzibar

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Zainab Chaula amewataka watendaji wa taasisi za mawasiliano zenye matawi Tanzania bara na visiwani kuwa wazi kwa wananchi kwa kutoa maelezo ya kina kuhusu sheria, taratibu na miongozo mbalimbali ili kuondoa sintofahamu kwa huduma zinazotolewa na taasisi hizo zilizo katika pande zote mbili za muungano ambazo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) pamoja na Shirika la Posta Tanzania (TPC).

Hayo ameyazungumza katika kikao cha Makatibu Wakuu wa Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (JMT)na Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kilichofanyika tarehe 8.3.2021 visiwani Zanzibar.

Dkt. Chaula ameongeza kuwa, taasisi hizo zinatakiwa kuzifahamu, kuzielewa na kuzifanyia kazi sheria, taratibu na miongozo mbalimbali ya utoaji wa huduma wanazozitoa ikiwa ni pamoja na kuelimisha jamii kufuata sheria hizo bila shurti.

“Tulikuwa na hoja nane baada ya kuzichambua zimebaki tano, ambapo kimsingi ni masuala ya kuweka sawa kanuni, taratibu na sheria zetu pamoja na kuongeza uelewa kwasababu lengo kuu la kuzitunga ni kuhakikisha kuwa zinafuatwa”, Dkt.Chaula

Aidha, amesema kuwa kikao kilikuwa kizuri na wataalamu walijipanga vema katika kufanya wasilisho ambapo changamoto mbalimbali zilizowasilishwa zimechukuliwa na kuboreshwa na zitawasilishwa katika kikao cha Mawaziri wa Wizara hizo mbili kwa lengo la kuzifahamu na kuzitolea maamuzi ili wananchi waendelee kufurahia muungano.

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi (SMZ) Amour Bakari amesema kuwa  kikao hicho ni muendelezo wa vikao vya mashirikiano  baina ya taasisi za mawasiliano za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambavyo awali vilianza katika ngazi ya watendaji.

“Kikao cha leo ni cha ngazi ya Makatibu Wakuu, na yale yote yaliyojadiliwa katika kikao hiki yatapelekwa katika kikao cha Mawaziri wa Wizara hizi mbili kitakachofanyika siku ya alhamisi ya tarehe 11.3.2021 hapa Zanzibar”, Amour Bakari

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalin

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari