Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Mhe. Mwita Waitara amesema kuwa dampo la pugu ambalo ni dampo kuu kwa Mkoa wa Dar es Salaam limeelemewa hivyo kunahaja ya kila Manispaa ya jiji la Dar es Salaam kuwa na dampo lake na kuacha kutegemea dampo la pugu ili kupunguza kero kwa wananchi walio karibu na dampo hilo.

Ameyasema hayo alipokuwa katika ziara ya ukaguzi wa mazingira katika  jiji la Ilala Mkoa wa Dar es Salaam amesema kuwa dampo hilo limekuwa likilalamikiwa sana na wananchi hasa kipindi cha masika, maji yanatiririka kutoka kwenye taka na kuingia katika makazi ya watu.

“Nimetembelea Manispaa zote za Mkoa wa Dar es Salaam Ubungo, Kinondoni, Kigamboni, Temeke na Nimemalizia hapa jiji la Ilala lakini nimewataka kila Manispaa wahakikishe wanadampo lao ili kuepusha adha kwa wananchi waliopo karibu na Dampo la Pugu. Hii ni njia bora ya kudhibiti kusambaa kwa taka Dar es Salaam” Waitara

Aidha Mhe. Waitara ameeleza kuwa taka zilizopo katika dampo la pugu zina changamoto zake kwani hazijatenganishwa kutoka kwenye chanzo hivyo kupelekea ugumu katika kuzichakata, ni vizuri wananchi wahakikishe wanatenganisha taka kuanzia kwenye chanzo ili kurahisisha zoezi hilo. Ameendelea kusema kuwa taka zikitenganishwa pia zinageuka kuwa fursa ya kujipatia kipato na sio taka tena

“Taka zilizopo hapa zimechanganyika kuna mifuko ya plastiki, vyuma na chupa ambavyo ingekuwa fursa katika kujipatia kipato na zisingekuwa taka tena kwani kunaviwanda vinauhitaji wa taka hizo kwa ajili ya kurejeleza. Hapa tulipofikia inabidi kuweka utaratibu ili eneo hili lianze kuwekwa miundombinu rafiki ili haya maji yasiende kwenye makazi ya watu na kusababisha kuathiri afya zao” Mhe. Waitara

Kwa upande wake Diwani wa kata ya pugu Mhe. Imelda Gerald amesema kuwa dampo kwa sasa ni kero japo meneja wa Dampo anajitahidi sana lakini kwa wananchi bado ni kero mvua inaponyesha maji machafu yanaenda kwa wananchi na kuathiri afya zao wanapata vipele, fangasi hata visima ukichimba maji yanakuwa machafu.

“Dampo la pugu limekuwa kero kwa wakazi lakini tunaomba pia magari yanayobeba taka yawe yamefunikwa ili kuepusha kudondosha taka karibu na makazi ya watu pamoja na magari yenyewe yawe mazuri maana kunamagari yanaletwa ni mabovu ambayo ni taka pia” alisema Bi Imelda

Vile vile Mhe. Waitara ametembelea Jengo jipya la Machinjio vingunguti na Machinjio ya Mazizini Gongolamboto kujionea hali ya kimazingira katika machinjio hayo. Mhe. Waitara amefurahishwa sana kuona jengo la machinjio la kisasa ambalo litakuwa rafiki kwa mazingira. Machinjio hayo bado hayajafunguliwa rasmi.

Mhe. Waitara pia alitembelea Machinjio ya Mazizini Gongolamboto na kubaini uchafuzi mkubwa wa Mazingira kwani machinjio hayo yanatiririsha maji machafu katika mfereji uliopo karibu na machinjio. Mhe. Waitara ameitaka NEMC kuchukua hatua za kisheria kuwajibisha Machinjio hayo mara moja

“Naagiza NEMC kuchukua hatua za kisheria kwa machinjio haya, kutiririsha maji katika mazingira ni kosa la kisheria hivyo wapigwe faini na onyo. Maji haya hayaruhusiwi kupelekwa kwenye mfereji au kwenye chanzo chochote cha maji bila kupimwa na kupewa kibali kutoka katika mamlaka husika” alisema Mhe. Waitara

Naibu Waziri alikuwa katika ziara ya siku tano katika Mkoa wa Dar es Salaam na amefanikiwa kutembelea Manispaa zote na kutoa maagizo katika kila Manispaa.