Samirah Yusuph.

Bariadi.
Penye miti hapana wajenzi,  ndivyo ambavyo unaweza kusema baada ya chuo cha ufundi Bariadi Dc kilichojengwa kwa thamani ya tsh milioni 180 na kiwanda cha kuchakata pamba cha Allience kisha kukabidhiwa kwa serikali kukosa wanafunzi.
Chuo hicho kinauwezo wa kuhudumia wanafunzi 200 Katika fani tano zilizosajiliwa chuoni hapo ambazo ni ufundi cherehani, ufundi seremala, ufundi Mwashi, kilimo pamoja na upishi.

Kwa sasa chuo hicho kina wanafunzi wa kike kumi na sita pekee katika fani ya ufundi cherehani huku fani nyingine zikiwa hazina wanafunzi.

Akizungumza na mwandishi wa habari mkufunzi Jeremiah Soga katika chuo hicho alieleza kuwa mwitikio wa vijana katika fani zilizopo chuoni hapo ni mdogo hivyo imewalazimu kuomba kusajili fani ya udereva na ufundi makenika ambazo zimekuwa ni chaguo la vijana wengi ili walau waweze kupata wanafunzi.

"Vijana wengi hawapendi kujifunza cherehani na wanaamini kuwa kazi ya kushona nguo ni ya kike pekee sababu inayo pelekea kuwa na wanafunzi wa kike...

Jamii pia haijapata muamko katika kuwaendeleza vijana ambao hawakupata nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari pamoja na wahitimu wa kidato cha nne pia wasichana ambao walikatiza masomo kwa sababu mbali mbali ikiwamo ujauzito shuleni pia wana nafasi sana hapa kwetu lakini hadi sasa wapo wachache tofauti na matarajio".

Baada ya chuo hicho kukabidhiwa kwa serikali Octoba, 2020 Mkuu wa Mkoa Anthony Mtaka alitoa nafasi ya bure kwa kinamama na wasichana waliokuwa wanatamani kuwa na ujuzi wa kushona nguo kujifunza bure kwa muda wa miezi mitatu.

Hatua ambayo ilipokelewa kwa mwitikio mkubwa na wananchi wa kata ya Kasori ambapo ndipo kilipo chuo hicho nu kudahili wanafunzi 98 Ambao walihitimu katika hatua ya awali.

Neema Sayi ni mhitimu wa mafunzo ya ushonaji yaliyofadhiriwa na mkuu wa Mkoa anaelezea kuwa fursa hiyo ilimpa nafasi ya kujifunza baada ya hapo hakuweza kuendelea tena kwa sababu ilitakiwa alipe ada ambayo ni tsh 120,000 Ili aweze kuendelea kujifunza.

Limi Batazali Ambaye ni mwanafunzi anaeleza lengo la kuwa katika chuo kuwa ni kujenga uwezi wa kujikwamua ki uchumi.

"Mafunzo yapo vizuri na imani ni kuwa baada ya mafunzo haya nitaweza kuendesha maisha yangu kupitia ujuzi ninao upata na nitakuwa fundi cherahani".

Baadhi ya wanafunzi hao wameeleza changamoto kubwa iliyopo kuwa ni upungufu wa walimu ambapo kuna walimu wawili pekee wote wakiwa ni wakiume

"Anahitajika mwalimu wa kike ili mwanafunzi anapokuwa na changamoto yoyote iwe ni rahisi kumfikia na kuzungumza nae...

Hatuna vitambaa vya kutosha, kuna uhaba sana wa vitambaa vya kujifunzia hali ambayo kidogo inatukwamisha kufikia malengo kwa wakati," alisema Gema Michael.

Afisa mtendaji katika kijiji cha Kasori Abdallah Bukagile alieleza namna ambavyo jamii imekipokea chuo hicho ambapo alisema kuwa bado kunachangamoto ya uelewa wa wazazi kupeleka watoto katika chuo hicho na tayari serikali ya kijiji imeanza mkakati wa kuhamasisha wazazi ili waweze kuelewa umuhimu wa kuwa na chuo hicho.

Huku baadhi ya wazazi wakieleza kuwa kuna vijana wengi ambao wapo mtaani bila kazi hivyo uwepo wa chuo hicho kitasabisha wajifunze ujuzi ili waweze kujiajiri wenyewe.

"Hapakuwahi kuwa na chuo katika maeneo haya kabla hivyo ni suala la muda ili kujipanga kupeleka wanafunzi...

Watu wakiona kuna wanafunzi wanahitimu na wanapata ujuzi watahamasika kwa sasa ni mwanzo, baada ya muda wengi watatamani wakajifunze," ameeleza Maduhu Masunga Mkazi wa kijiji cha Kasori.

Licha ya kutokufikia malengo ya ujenzi wa chuo hicho, Mkurugenzi mkuu wa kiwanda kilichojenga chuo hicho Boaz Ogola alionyesha kutokukata tamaa kuendelea kuisaidia jamii hiyo katika upande wa Elimu ili vijana waweze kuelimika na kuajiriwa au kujiajiri wenyewe.

" Wananchi bado wanahitaji elimu ili waweze kuelewa kwa nini chuo kipo katika mazingira yao...

Muitikio wa elimu upo chini lakini tunahitaji wananchi wahamasike zaidi ili waelewe umuhimu wa vijana kuwa na elimu".

Kwa upande wake mkuu wa Wilaya ya Bariadi Festo Kiswaga alifafanua kuwa chuo hicho kimesajiliwa, changamoto zilizopo ni kwa sabababu hakuna wanafunzi pindi watakapo kuwa wakiongezeka walimu watakuwepo kuendana na idadi ya wanafunzi.

" Mafunzo ya udereva yameonekana kuwa yanahitajika zaidi hivyo wilaya ipo katika hatua za mwisho kupeleka magari pale ili wananchi wapate wanacho kihitaji".

Mwisho.