Bunge la Libya limeiidhinisha serikali mpya ya mpito ya umoja wa kitaifa itakayoliongoza taifa hilo la Afrika Kaskazini lililoharibiwa kwa vita kuelekea uchaguzi uliocheleweshwa kwa muda mrefu unaopangwa mwishoni mwa mwaka huu.
Spika wa bunge Aguila Saleh amesema wabunge 132 wamepiga kura ya imani ya kuunga mkono serikali iliyopendekezwa na kaimu Waziri Mkuu Abdul-Hamid Mohammed Dbeibeh.
Amesema muhula wa serikali hiyo utakamilika Desemba 24 wakati ambapo uchaguzi wa rais na bunge utafanyika. Kura hiyo imepigwa katika siku ya tatu ya mdahalo wa bunge katika mji wa pwani wa Sirte.
Serikali hiyo ya mpito itachukua nafasi ya serikali ya umoja wa kitaifa iliyoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, ambayo ilikuwa ikiudhibiti mji mkuu Tripoli na maeneo ya magharibi, pamoja na serikali ya upande wa mashariki inayohusishwa na mbabe wa kivita Khalifa Haftar.