Biteko: Kamati Ya TEITI Inawajibu Wa Kuitangaza Taasisi Hiyo
Tito Mselem na Godwin Msabala
Imeelezwa kuwa, wajumbe wa Kamati ya Taasisi ya Uwazi na Uhamasishaji katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi Asilia (TEITI) wana wajibu wa kuitangaza TEITI ili kuifanya ijulikane ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini Doto Biteko kwenye kikao chake na Wajumbe wa Kamati ya TEITI kilichofanyika Machi 10, 2021 katika Ukumbi wa Samwel Sitta uliopo katika Ofisi za Bunge jijini Dar es Salaam.
Waziri Biteko amesema kuwa, mwenyewajibu wa kuifanya TEITI ijulikane ni TEITI wenyewe ambapo ameitaka taasisi hiyo kujitangaza ili wananchi waweze kujua kazi na majukumu ya Taasisi hiyo.
“Kila mjumbe ana wajibu wa kuwa na msukumo chanya ambao utaifanya Taasisi hii kufurukuta na kujiweka hadharani ionekane,” amesema Waziri Biteko.
Akizungumza kwenye kikao hicho, Waziri Biteko amesema kuwa, TEITI iko nyuma kwa maana ya kujulikana ambapo amesema TEITI inapaswa kuwa maktaba na kimbilio la taasisi nyingine kwa sababu, inatakiwa kuwa na jicho la kuona kitaifa na kimataifa litakaloona na kusaidia maendeleo ya uziduaji nchini hasa katika Rasilimali Madini, Mafuta na Gesi asilia.
Aidha, Waziri Biteko, ameitaka Taasisi ya TEITI kuhakikisha inafuatilia ili kujua na kujiridhisha mipango na gharama iliyotengwa na migodi wanapotaka kufunga migodi hiyo na piay kukagua mazingira yanayozunguka migodi hiyo kujihakikishia kuwa mazingira hayo yanaachwa katika hali nzuri kwani kuna mahusiano makubwa kati ya mazingira na wananchi wanaotegemea hayo mazingira katika maisha yao ya kila siku.
“Naomba nichukue fursa hii kuisisitiza kamati hii kuhakikisha anafanya ziara za mara kwa mara katika migodi yetu hapa nchini ili mjiridhishe na mjionee namna shughuli na biashara za madini, mafuta na gesi asilia zinavyofanyika, pia mazingira yanayozunguka migodi yako katika hali nzuri,’’ alisema Waziri Biteko.
“Nataka niwahakikishie kamati ya TEITI kwamba, sisi kama Wizara ya Madini tuko tayari kuwapatia kiasi chochote cha fedha mtakazo hitaji lakini lazima mtuletee matokeo chanya,” aliongeza Waziri Biteko.
Pia, Waziri Biteto amemtaka mwenyekiti wa TEITI kuisimamia sekta hiyo ya Uziduaji ili ijulikane na ilete matokeo chanya kwa taifa na kimataifa.
Naye, Mwenyekiti wa Kamati ya TEITI Ludovick Utouh, amempongeza Waziri Biteko kwa kuonesha nia ya kuisadia Taasisi hiyo, ambapo amesema, taasisi ya TEITI itaendelea kutambua mchango wa Wizara ya Madini katika kuchangia maedeleo ya Taasisi hiyo.
Aidha, Utouh, amesema kuwa, Kamati ya TEITI ipo tayari kupokea maagizo na maelekezo ya Waziri Biteko na kuwataka wajumbe wote kuwa wazalendo ili walete maendeleo kwa taifa lao.
Kwa upande wake Makamu Katibu Mtendaji wa TEITI Mariam Mgaya amesema, TEITI itaendelea kuhakikisha kuwa, Serikali inaweka mifumo ya uwazi katika usimamizi wa rasilimali madini, mafuta na gesi asilia ili kuboresha ukusanyaji wa mapato na manufaa yanayotokana na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa rasilimali hizo.
Aidha, Mgaya amesema, kwa kiwango kikubwa ripoti za TEITI zinahusisha uwekaji wazi wa taarifa za kampuni kubwa na za kati tu, lakini kwa sasa TEITI imepanga kuweka wazi mapato na taarifa nyingine za wachimbji wadogo.
Aidha, Mjumbe wa Kamati ya TEITI Dkt. Camilius Kassala, amesema maendeleo chanya ni chachu katika kupiga hatua na kusonga mbele kimaendeleo, ambapo ameeleza kuwa utangulizwe uzalendo mbele ili kuleta maendeleo endelevu ya taifa.