Rais Joe Biden wa Marekani siku ya jana aliufungua mkutano na viongozi wa mataifa ya Australia, India na Japan akiahidi kufanya kazi pamoja na washirika wao kuimarisha uthabiti kwenye kanda ya India na Pasifiki. 

Mkutano huo kwa njia ya video unaowajumuisha Biden na mawaziri wakuu wa Australia, India na Japan unafanya katika wakati Washington inatafuta njia ya kukabili nguvu za kiuchumi na kijeshi za China. 

Biden amewaambia viongozi wenzake kuwa kanda huru ya India na Pasifiki ni muhimu kwa ustawi wa pande zote na kuhimiza ulazima wa kuimairisha ukuaji wa uchumi wa ndani na ule wa ulimwengu. 

Pamoja na mambo mengine, mkutano huo utatangaza makubaliano ya kifedha ya kuzalisha chanjo zaidi za virusi vya corona, ushirikiano katika sekta ya viwanda pamoja na uzalishaji wa bidhaa.