Mataifa kadhaa ya Ulaya yamesimamisha kutumia chanjo ya COVID-19 ya AstraZeneca, baada ya ripoti kuwa chanjo hiyo ilisababisha kuganda kwa damu miongoni mwa baadhi ya watu walioipokea. 

Denmark, Iceland na Norway ni miongoni mwa nchi hizo zilizochukua hatua hiyo ya tahadhari. 

Hata hivyo, mataifa hayo yalijizuia kusema moja kwa moja kuwa chanjo hiyo ndio sababu ya tatizo hilo la kuganda kwa damu. Denmark imesema itasitisha utoaji wa chanjo ya AstraZeneca kwa siku 14, na waziri wake wa afya Magnus 

Heunicke amesema kwa wakati huu hawawezi kusema kwa uhakika kuwa chanjo hiyo ina uhusiano na tatizo hilo la damu. 

Mtaalamu wa tiba ya maradhi yanayosababishwa na virusi kutoka taasisi ya magonjwa ya kitropiki iliyoko mjini London, Polly Roy, ameiambia DW kuwa huwenda tatizo hilo halina uhusiano na chanjo yenyewe, bali matatizo waliyokuwa nao wagonjwa walioathirika.