Kampuni inayotenegeneza chanjo ya AstraZeneca imesema inaheshimu uamuzi wa Ujerumani wa wiki hii wa kusimamisha matumizi ya chanjo hiyo kwa baadhi ya watu wake, japo imesisitiza kuwa chanjo hiyo imethibitishwa kuwa salama na taasisi zingine za afya. 

Kampuni za utengenezaji dawa za Uingereza na Sweden zinazoshirikiana kutengeneza chanjo za Oxford/AstraZeneca kwenye taarifa yao ya pamoja, zimesema zimekubaliana na uamuzi uliochukuliwa na Ujerumani lakini zimeongeza kusema kuwa watafiti wanaochunguza usalama wa chanjo za Covid-19 kutoka Uingereza na Umoja wa Ulaya hawakuweza kuthibitisha uhusiano wowote kati ya matumizi ya chanjo hiyo na matatizo ya kuganda damu. 

Wizara ya afya ya Ujerumani imetangaza kuwepo uangalifu katika matumizi ya chanjo ya AstraZeneca kwa watu wenye umri wa chini ya miaka 60 na pia kwa wale walio na miaka 60 na zaidi kutokana na wasiwasi wa kuganda kwa damu kwenye ubongo.