Mwenyekiti wa Tume ya uchunguzi kuhusu madai ya rushwa yanayomkabili aliyekuwa rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, amesema anataka kiongozi huyo wa zamani kuhukumiwa kifungo gerezani kwa kushindwa kufika mahakamani kujibu madai ya ufisadi yanayomkabili.

Jaji Ray Zondo anamshtumu Jacob Zuma kuidharau mahakama baada ya kudharau ombi la kufika mbele ya tume ya uchunguzi anayoongoza.

Hata hivyo Jacob Zuma amebaini kwamba jaji Zondo si mtu mzuri kwani alionyesha upendeleo katika uamuzi alioutoa dhidi yake.

Wakati huo huo jaji Ray Zondo amesema yuko tayari kuomba mahakama ya juu ya nchini Afrika Kusini kumhukumu aliyekuwa rais kwa kosa la kuidharau mahakama kwa kitendo chake cha kukaidi wito wa kufika mahakamani.

Mahakama ya kikatiba mwezi uliopita, ilitoa uamuzi wake na kusema kuwa Bwana Zuma analazimika kufika mbele ya tume hiyo.

Zuma anashtumiwa kuwa wakati wake madarakani, aliruhusu familia tajiri ya Gupta kupora mali ya serikali na kushawishi sera na uteuzi wa mawaziri. Madai ambayo Zuma anaendelea kukanusha.