Wizara Ya Kilimo Na Mkakati Wa Kukuza Tija Katika Kilimo- Prof. Mkenda
Wizara ya Kilimo imesema iko katika utekelezaji wa mikakati ya kuongeza tija na kuhakikisha wakulima wananufaika na shughuli za kilimo ikiwemo uhakika wa masoko ya mazao.
Waziri wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda amesema hayo leo asubuhi (11.02.2021) wakati akizungumza kwenye kipindi cha Kumekucha kinachorushwa na kituo cha ITV akiwa jijini Dodoma
Prof. Mkenda amesema kwa sasa bado kilimo kinachangia chini ya asilimia 30 kwenye pato la Taifa wakati ikiwa imeajili zaidi ya asilimia 70 ya nguvu kazi hali inayochangiwa na kuwepo tija ndogo kwenye kilimo.
“Tija bado ni ndogo sana katika kilimo hali inayosababisha wakulima walime eneo kubwa wakati mavuno wanayopata ni kidogo ,hivyo wizara tunajielekeza kukuza tija mfano sasa tunazalisha wastani wa tani 0.7 za ngano kwa hekta tofauti na wenzetu waliofikia tani 5.0 kwa hekta hali inayosababisha tuagize zaidi ya tani 800,000 za ngano toka nje ” alisisitiza Mkenda.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkenda amesema wizara inaendelea kutekeleza kauli ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli kutaka kuona mkulima ananufaika na kilimo.
“Wizara inatekeleza agizo la Rais Dkt. Magufuli la kuhakikisha mkulima ananufaika na kilimo chake kwa kuondoa kero na changamoto zinazokwamisha ikiwemo uhakika wa masoko ya mazao” alisema Prof. Mkenda.
Alipoulizwa kuhusu changamoto za wizara kwa sasa ,Prof. Mkenda alisema wizara inakabiliana na tatizo la wakulima wa tumbaku kukosa soko la mazao yao wakati makampuni yanayonunua zao hilo huuza kwa bei ubwa kwenye nchi za nje .
Mkenda amesema baadhi ya makampuni ya tumbaku nchini hununua zao hilo kwa bei ya chini wakidai ni ya kiwango cha chini (makinikia) kisha huyapeleka nje na kuuza kwa bei nzuri.
“Suala la makinikia ya tumbaku halikubaliki sasa, serikali itahakikisha kunakuwepo ushindani wa kweli katika masoko ya tumbaku ili wakulima wetu wanufaike tofauti na ilivyo sasa” alisisitiza Prof. Mkenda.
Kuhusu suala la upatikanaji sukari nchini Prof. Mkenda alisema serikali imeanza kuchukua hatua za kudhibiti uagizaji sukari toka nje ya nchi kupitia makampuni ambayo ndio wazalishaji.
Aliongeza kusema tatizo la upungufu wa sukari nchini linachangiwa na viwanda kushindwa kuongeza uwezo wake wa kuchakata miwa yote ya wakulima
“Upungufu wa sukari nchini haukufanywa na upungufu wa miwa tatizo ni makampuni /wawekezaji kutokuongeza uwezo wa kuchakata miwa yote ya wakulima” alisema Mkenda
Waziri huyo wa kilimo amesema baada ya mwaka huu serikali haitotoa vibali kwa wawekezaji waliopewa viwanda vya sukari kuagiza sukari nje badala yake kazi hiyo itafanywa na Bodi ya Sukari Tanzania.
Takwimu za wakulima wa miwa wa wilaya ya Kilombero kwa mwaka 2019/20 zilionyesha walizalisha wastani wa tani 900,000 za miwa wakati uwezo wa kiwanda cha sukari Kilombero ni kuchakata tani 600,000 hali iliyosababisha miwa taribani tani tani 300,000 kukosa soko na kuharibika.
Kwa upande wa zao la ngano Prof. Mkenda amesema tayari mkakati wa kuhakikisha zao hilo linalimwa kwa wingi umepatikana kwa serikali kusaini makubaliano na wafanyabiashara wakubwa wa ngano kununua asilimia 60 ya mahitaji yao ya ngano toka nchini.
“Tumekubaliana na wafanyabiashara wakubwa wa ngano kuwa kabla hujaleta ngano toka nje mfano ikiwa unaingiza asilimia 60 basi utalazimika kununua asilimia 60 ya ngano inayozalishwa ndani ya nchi hatua itakayosaidia kukuza soko la wakulima wetu” alisema Prof. Mkenda.
Ili kufanikisha mkakati huo wa kukuza tija kwenye kilimo, Prof. Mkenda ametaja mambo manne ya kipaumbele kwanza kuhakikisha nchi inazalisha mbegu bora zilizotafitiwa na wataalam wazalendo zikiwemo zile za asili.
Pili, kuendelea kutoa elimu ya kilimo bora ili wakulima wawe na uwezo wa kuzalisha mazao bora kwa kutumia pembejeo na mbegu bora kwa wakati na tatu,wizara itahakikisha masoko ya mazao yanapatikana kwa wakati ndani na nje ya nchi.
Nne alisema wizara ya kilimo inaendelea kutafuta namna bora ya kuwezesha upatikanji wa mitaji ikiwemo mikopo yenye masharti na riba nafuu kwa wakulima na wawekezaji kwa kuzungumza na Wizara ya Fedha na taasisi za kifedha za ndani na nje ya nchi.