Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Prof. Adolf F. Mkenda amesema Serikali haitotumia amri na matamko kuwafanya wafanyabiashara wa mazao ya kilimo nchini kuongeza ufanisi bali itashirikana nao kukuza fursa za masoko ya biashara hiyo nchini.

Waziri Prof. Mkenda ametoa kauli hiyo leo Jijini Dodoma wakati alipofungua mkutano wa Wizara na wafanyabiashara wa mazao ya nafaka unaolenga kujadili fursa za masoko ya mazao ya nafaka ndani na nje ya nchi pamoja na kuweka mikakati ya kutatua changamoto zinazowakabili. Mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli la kutaka wakulima wapate masoko ya uhakika na wafanyabiashara wa mazao ya nafaka nchini wawe na fursa ya kukuza uchumi.

Prof. Mkenda ameeleza kuwa Wizara ya Kilimo tayari imeanza kutekeleza mikakati mbalimbali ikiwemo kuhakikisha upatikanaji masoko ya uhakika kwa wakulima wa mazao ya zabibu, ngano na mazao ya nafaka ili kupunguza utegemezi wa kuagiza malighafi za kuzalisha bidhaa kutoka nje ya nchi.

“Tunataka mfanyabiashara anayetengeneza juisi au mvinyo kwanini aagize malighafi toka nje wakati Tanzania tunayo ardhi nzuri na watu wenye uwezo wa kulima mazao hayo. Ndio maana tumewaita hapa tujadiliane namna ya kukuza masoko ya mazao yetu ya ndani ikiwemo nafaka” alisisitiza Prof Mkenda.

Kuhusu mazao ya nafaka Prof. Mkenda alisema kati ya kipindi cha mwaka 2015 – 2020, Tanzania ilisafirisha wastani wa tani 105,119 za mahindi katika nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, DRC, Zambia, Malawi na Msumbiji ikilinganishwa na wastani wa tani 1,103,522 zilizoingia katika nchi hizo sawa na asilimia 10. Vilevile, katika kipindi hicho, Tanzania ilisafirisha wastani wa tani 66,818 za mchele katika nchi hizo ikilinganishwa na wastani wa tani 1,661,743 zilizoingia katika nchi hizo sawa na asilimia 4. Kwa takwimu hizi Prof.Mkenda amesema zinaonesha  kwa kiasi gani kama nchi hatujaweza kutumia vizuri fursa za masoko katika nchi zinazotuzunguka.

Katika hatua nyingine Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Dotto James amewaambia wafanyabiashara ya mazao ya nafaka kuwa serikali tayari imefanikiwa kufuta na kuondoa kodi na tozo kero zaidi ya 250 kwa lengo la kuweka mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara ikiwemo wa mazao ya nafaka kukuza uchumi wa nchi.

Bw. Dotto aliongeza kusema serikali inataka kuona kilimo kinafungamanishwa na viwanda ili kuongeza thamani ya mazao na kuwezesha kupatikana uhakika wa masoko ya mazao ili kufikia mapinduzi ya viwanda.

“Sina shaka na Wizara ya Kilimo sasa hivi tumeanza kuona mwanga, tunaelekea vema kukuza uchumi wa nchi kupitia sekta ya kilimo “ alisema Dotto.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Dkt. Christine Ishengoma alisema Bunge linaamini kuwa mkutano huu utazaa matunda makubwa kwa wakulima na wafanyabiashara ambapo changamoto za masoko zitapata ufumbuzi.

Wizara ya Kilimo imeandaa mkutano huo wa siku moja uliohusisha wakuu wa mikoa, wabunge, mabalozi wanaowakilisha Tanzania nje ya nchi, taasisi za fedha na wafanyabiashara wa ndani zaidi ya mia moja.


Mwisho
Imetolewa na;

Revocatus A. Kassimba
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini