Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Mwigulu Nchemba ameagiza vyombo husika kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaosambaza taarifa za uongo mitandaoni kuhusu afya za watu wengine.

Dkt. Nchemba amesema hayo kufuatia uwepo wa uvumi mwingi mitandaoni kuhusu hali za afya za watu mbalimbali huku akifafanua kwamba, kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mitandao kinazuia watu kutoa taarifa za uongo.

Kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Instagram, Dk Mwigulu amesema, “Taifa lipo kwenye msiba wa viongozi wetu waliotangulia mbele ya haki kwa mapenzi yake Mungu. Kumetokea tabia mbaya ya kuzushiana kwamba fulani anaumwa, na fulani naye anaumwa.”

“Mara nasikia fulani amekufa na fulani naye amekufa. Huku ni kukosa utu ni kuathiri maisha binafsi ya mtu, familia yake na kusababisha taharuki kwenye jamii. Kifungu cha 16 cha Sheria ya Mitandao kinazuia watu kutoa taarifa za uongo. Nimeelekeza vyombo vyote husika kuchukua hatua bila kusubiri mtu binafsi akalalamike. Nani amekupa kazi ya kufuatilia afya za wengine na kuwa msemaji wa hali zao? Tuache tabia hii mara moja.” Mwigulu