WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka watumishi wa umma wasikate tamaa kwa vile mishahara mipya haijatangazwa na badala yake amewasihi waendelee kuchapa kazi kwani maslahi yao yanaendelea kuboreshwa.

“Nitoe wito kwa watumishi wa umma, wasikate tamaa kwa sababu mishahara mipya haijatangazwa, kikubwa waendelee kuwasilisha hoja zao kupitia mabaraza yao ya wafanyakazi,” amesema.

Waziri Mkuu ametoa wito huo jana (Alhamisi, Februari 11, 2021) wakati akijibu swali la mbunge wa Konde, Bw. Khatibu Said Haji (ACT-Wazalendo) katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu bungeni jijini Dodoma. Mbunge huyo alitaka kujua ni lini wafanyakazi wa Tanzania watapandishiwa mishahara na kuboreshewa maslahi yao.

“Serikali inayo dhamira na inaendelea na suala la kuboresha maslahi ya watumishi wa umma. Serikali ya awamu ya tano ilipoingia madarakani ilibaini kwamba ukitangaza kupandisha mishahara, unawaumiza watu wengi wakiwemo wakulima, wafugaji na wavuvi kwani gharama za bidhaa hupandishwa haraka sana.”

Amesema Serikali imejifunza kuwa inapotangaza hadharani kuhusu kupandishwa mishahara, imekuwa inasababisha ugumu wa maisha kwani huduma nyingine kwenye masoko ama usafiri wa mabasi zote zinapanda.

Waziri Mkuu amesema maslahi ya watumishi wa umma hayapo kwenye mshahara peke yake bali pia yanaboreshwa kwa kupunguza kodi na kuwapandisha madaraja. “Mheshimiwa Rais Magufuli alisema kupandisha mshahara kwa sh. 20,000 au 30,000 haina tija kwa mtumishi bali kupunguza kodi kunamsaidia zaidi mfanyakazi,” amesema.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali inapotwaa ardhi ni lazima pafanyike tathmini ili kujua eneo husika lina thamani gani kulingana na mali zilizopo iwe ni nyumba, mazao au kiwanda.

Ametoa kauli hiyo wakati akijibu swali la mbunge wa viti maalum (CHADEMA), Bi. Esther Matiko kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu bungeni. Mbunge huyo alitaka kujua ni kwa nini tathmini zinazofanyika hazikamiliki na wananchi wakalipwa fidia ili waende sehemu nyingine wakaendelee na shughuli zao.

Waziri Mkuu amesema ardhi ni mali ya Serikali lakini kila mtu anapaswa kuwa na hati ya kutambulisha matumizi ya ardhi anayoimiliki. “Kila mtu anapaswa kuwa na hati ya kubainisha ardhi anayoimiliki ni ya kitu gani, iwe mashamba, kujenga nyumba au kiwanda,” amesema.

“Kwa hiyo, Mheshimiwa Mbunge kama unalo eneo ambalo wananchi wana malalamiko, ni vema uyafikishe kwa viongozi wa eneo husika ili utaratibu wa fidia ufanyike,” amesema.