Tito Mselem na Steven Nyamiti, Dodoma
 Waziri wa Madini Doto Biteko ameitaka Bodi ya Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini (GST) kujitathimini namna ya utendaji kazi wao.

Waziri Biteko ameeleza kuwa, GST inapaswa ijitangaze ili jamii itambue kazi ya Taasisi hiyo ambapo amesisitiza shughuli zinazofanywa na Taasisi hiyo lazima zitambulike ndani na nje ya nchi.

“Taasisi yoyote inayokua, ikiwa Taasisi inayosubili matukio yaiibue, basi Taasisi hiyo maisha yake ni mafupi, mimi naiona hatari ya GST, utendaji kazi wa Taasisi hii bado hauridhishi ninatamani kuiona GST ikizungumzwa” amesema Biteko.

Waziri Biteko amesema kuwa, Uti wa Mgongo wa Sekta ya Madini ni GST ambao ndio watafiti wa madini nchini ambapo amewataka wajumbe wa Bodi ya GST wabuni mikakati madhubuti itakaiyoboresha Taasisi hiyo ili kuifanya GST ijiendeshe yenyewe.

Aidha, Waziri Biteko ameongeza kuwa, anatamani kuona mabadiliko ya Sekta ya Madini nchini yanaenda sambamba na ukuaji wa Taasisi ya GST.

“Kiu yangu ni kuiona GST inakua na inajiendesha yenyewe ikiwa ni pamoja na kuongeza mapato zaidi tofauti na ilivyo sasa,” amesema Waziri Biteko.

Pia, Waziri Biteko amesema, GST inatakiwa ijitangaze ndani na nje ya nchi ambapo ameitaka Bodi hiyo ishiriki kikamilifu katika Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta Madini utakaoanza Februari 21 mpaka 24, 2021 ili kutumia fursa hiyo kujitangaza kimataifa.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Madini Prof. Simon Msanjila ameipongeza GST kwa kushiriki uchunguzi wa upatikanaji wa madini ya Urenium Mvomero Mkoani Morogoro ambapo mpaka sasa matokeo ya tafiti hizo yametoka na yapo katika hatua ya kujadiliwa

Awali, akifungua Mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi ya GST Prof. Justinian Ikingula alianza kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa kuiwezesha GST kutimiza majukumu yake.

Akifafanua juu ya uwezeshaji huo Prof. Ikingula alisema kuwa serikali imeipatia GST kiasi cha Shilingi bilioni 3.3 ambazo zimewezesha GST kununua vifaa mbalimbali vya maabara ikiwa ni pamoja na ununuzi wa magari sita ambayo yatarahisisha utendaji kazi wa Taasisi hiyo.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya GST, Prof. Ikingula alieleza Kuwa GST imeshiriki katika tafiti mbalimbali za jiosayansi kama vile utafiti katika mji wa serikali (Mtumba), Mradi wa Ujenzi wa reli ya mwendokasi pamoja na mradi wa Bwawa la uzalishaji umeme lijulikanalo kwa jina la (Mwalimu Nyerere Hydro Power).