Na. Catherine Sungura,WAMJW-Kibaha
“Huduma za Uuguzi na Ukunga zinapimwa zaidi na uadilifu wa watoa huduma, uadilifu unasaidia kuzingatia matumizi sahihi ya elimu aliyonayo mtaaluma kwani elimu bila maadili ni Bure”.
 
Hayo yamebainishwa jana Kwenye hotuba ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi wa Idara ya Uuguzi na Ukunga Bi. Ziada Sellah wakati wa hafla ya kwanza ya kuwasajili Wauguzi na Wakunga wapya iliyofanyika Kwenye ukumbi wa kituo Cha Maendeleo ya Uuguzi na Ukunga mjini Kibaha.
 
Bi.Sellah amesema kuwa wanataaluma hao wanapaswa kuzingatia viapo vyao vya taaluma na kutoa huduma kwa kujali utu, heshima na upendo kwa wagonjwa ambao wanawahudumia katika vituo vyao vya kazi.
 
“Tukio hili la Leo litasaidia kutoa msisitizo kwa wanataaluma kutambua wajibu wao katika utoaji wa huduma huku wakizingatia maadili ya taaluma zao, kitendo hiki kilitakiwa kutekeleza kipindi kirefu kilichopita na ni vyema kikatekelezwa na taaluma zote za sekta ya afya nchini ili kuwafanya wahitimu kuheshimu taaluma zao”. Amesisitiza Mkurugenzi Sellah.
 
Kwa upande wa kuboresha uwezo wa kutekeleza majukumu ya Baraza la wauguzi na Wakunga nchini, Bi.Sellah amelitaka Baraza hilo kuzingatia ubora wa stadi na maadili ya taaluma ili kushuhudia mabadiliko makubwa ya ubora wa huduma za afya nchini.
 
“Tumeendelea kushuhudia changamoto nyingi za huduma zinazotolewa bila kuzingatia maadili ikiwa ni pamoja na kunyanyaswa wateja, natoa msisitizo tena kwa wanataaluma wote wa sekta ya afya zingatieni viapo vyenu”. Ameongeza Bi. Sellah.
 
Vilevile Bi. Sellah amewahimiza viongozi katika ngazi za mikoa na hospitali za Rufaa ambao wamepewa mamlaka na Sheria ya Uuguzi na Ukunga ya mwaka 2010 kuchukua hatua za mapema pale panapobainika Kuna upungufu katika utoaji wa huduma.
 
“Tekelezeni majukumu yenu kwa haraka iwezekanavyo na kisha mtoe  taarifa kwa Baraza la Uuguzi na Ukunga makao makuu kwa hatua zaidi, wateja wanapenda kushuhudia haki inapatikana mapema, kuchelewa kuchukua hatua panapotokea upungufu kunaleta picha mbaya kwa wateja na kuleta taswira kuwa Kuna kulindana au udhaifu katika usimamizi wa maamuzi”.
 
Bi. Sellah amelipongeza Baraza hilo kwa kuandaa tukio hilo na kuwahimiza liwe endelevu kwa vile linatoa wasaa kwa wanataaluma kuelewa maana ya Baraza na majukumu yake pia amewasisitiza kuhusu maadili ya taaluma yao.
 
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Bw. Abner Mathube amesema Sheria iliyounda Baraza hilo ilitungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa lengo la kuhakikisha  watanzania wanapata huduma za Uuguzi na Ukunga zilizo salama hivyo Baraza hilo limehakikisha linawasajili wataalamu wenye sifa za kitaaluma na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa Sheria wale ambao wanatoa huduma chini ya viwango vinavyotegemewa.
 
Wakati huo huo Kaimu Msajili wa Baraza la Uuguzi na Ukunga Bi. Happy Masenga amesema Baraza linahakikisha leseni ya kutoa huduma za kitaaluma za Uuguzi inatolewa kwa waombaji waliopitia mafunzo yaliyokubalika kutoka vyuo vinavyotambulika na kufaulu mitihani ya usajili inayoendeshwa na Baraza.
 
Bi. Masenga amesema toka mwaka 2014 Baraza limekuwa likiendesha mitihani ya usajili na leseni ili kupima umahiri wa wahitimu kwa lengo la kujiridhisha kama wanao uwezo wa kutoa huduma salama kwa wateja na hadi sasa wahitimu 30,715 wamekwishafanya mitihani hiyo.
 
Katika hafla hiyo jumla ya wauguzi na Wakunga 839 waliohitimu masomo ya Uuguzi na ukunga katika ngazi mbalimbali na kufaulu mitihani ya usajili na leseni iliyofanyika Novemba, 2020 na mahafali hayo yaliyoandaliwa na Baraza yamefanyika kwa Mara ya kwanza tangu Baraza hilo kuanzishwa mwaka 1953.