Na. Catherine Sungura, WAMJW-Dodoma
Wauguzi Viongozi wa vituo vya kutolea huduma za afya nchini wametakiwa kuhakikisha wanajadili sababu zinazochangia kuzorota kwa huduma kwa wateja hali ambayo husababisha kuongezeka kwa malalamiko ya mara kwa mara  kutoka kwa wateja  wanaofika kupata huduma za afya kwenye vituo vyao.

Maelekezo hayo yametolewa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima wakati akifungua mkutano wa siku mbili  wa wauguzi viongozi unaofanyika jijini Dodoma.

Dkt. Gwajima amesema wauguzi ni rasilimali na nguvu kubwa katika sekta ya afya nchini na duniani kwani ni watoa huduma ya afya ambao wako mstari wa mbele katika kutoa huduma wakati wote kwa kuwahudumia wangonjwa  na wateja  wenye huitaji bila kuchoka.

“Tufike mahali tuwakatae wale wanaosababisha malalamiko kwa wateja, tubadilike,ni wazi kwamba wauguzi na wakunga kwa umoja wenu na kutumia taaluma,  ujuzi na weledi wenu mnaweza mkatupa majibu ya kwanini huduma kwa wateja katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini zinakuwa na changamoto kiasi cha kuleta malalamiko kwa baadhi ya wateja wetu”. Alisisitiza

Aliongeza kuwa ili kuweza kutatua changamoto hizo ni vyema kufufuliwa kwa kamati za maadili za wauguzi ili kuweza kukaa pamoja na  kujadili malalamiko yanayowakabili na kuzitafutia njia ya kuzitatua.

“Ninyi ndio mnaojua suala zima la utoaji za afya na mtakao fanya sekta ya afya iende mbele ila wapo wachache wenu ambao wanaharibu taaluma hii,kwahiyo mnaweza kuwarekebisha kwani wauguzi mnaaminika  hivyo inaonesha umuhimu wenu kwenye sekta hii”. Alisema Dkt. Gwajima

Hata hivyo Waziri huyo aliwataka wauguzi, wakunga na watoa huduma wengine wote katika sekta ya afya  kutoa huduma zinazozingatia utu, heshima na upendo kwa wagonjwa  kwani wao wanatakiwa kuwa mstari wa mbele  katika kuwajali na kuwatunza  wagonjwa  na kuwahudumia kwa utaalam,weledi , ubunifu na mtazamo chanya kwa kifuata maadili ya taaluma zao na miongozo ya wizara ya afya.

Naye Mkurugenzi wa huduma za Uuguzi na Ukunga kutoka Wizara ya Afya Bi. Ziada Sellah amesema kuwa mkutano huo utajadili ubora wa huduma za kiuguzi na ukunga na mbinu za kuongeza uzalishaji katika sekta ya afya ili kuondoa kushuka kwa viwango vya huduma za uuguzi na ukunga  hasa katika maeneo ya kutolea huduma  pamoja na kuongeza kujituma na kujitoa zaidi katika utoaji huduma ili kumsaidia muuguzi kumjua kila mgonjwa na kumhudumia ipasavyo.

Aliongeza kwamba mkutano huo utawakumbusha majukumu muhimu katika utendaji kazi hasa kwa kuihakikisha zinasimamiwa kwa ushirikiano katika ngazi zote “tutatumia wasaha huu kujadili changamoto ambazo zimekuwa zikiathiri ubora wa huduma na kuleta malalamiko kwenye jamii hususan suala la uzingatiaji wa utu, heshima, upendo na maadili ili kuimarisha huduma kwa wateja.

Bi. Sellah amesema baada ya mkutano huo  wanatarajia  kuja na majibu thabiti  ili kuweza kutatua changamoto kubwa kwa kuzingatia nchi inaelekea kwenye mpango wa bima ya afya kwa wote.

Wakati huo huo Afisa Muunguzi Mkuu anayesimamia  huduma za Uuguzi na Ukunga nchini  pamoja na afya ya uzazi  wa mama na mtoto kutoka TAMISEMI Bi.Dina Atinda amesema ofisi ya Rais TAMISEMI imepokea maelekezo yaliyotolewa na Wizara ya afya na kuahidi kuyafanyia kazi kama wasimamizi wa watoa huduma za afya na hivyo kuwataka wauguzi  kufanya kazi kwa kufuata maadili na upendo ikiwa ni pamoja na kutoa  huduma bora kwa wateja/wagonjwa ili kuepuka malalamiko na hivyo kuwatendea haki wananchi wanaofika kwenye vituo vyao vya huduma za afya.

Kwa upande wa viongozi  amewata kusimamia wauguzi katika ngazi zote ili wauguzi waweze kufanya vizuri kwa kufuata maadili na kuelekeza kufufua kamati za maadili na kukaa kwa pamoja kujadili utendaji kazi wao wa kila siku na wale wanaoshindwa basi kuwapeleka kwenye mabaraza ya kitaaluma.