Watu wasiopungua 60 wamefariki dunia kufuatia ajali ya boti magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Steve Mbikayi, Waziri wa Masuala ya Kibinadamu wa nchi hiyo amesema boti hiyo iliyokuwa imebeba abiria kupita kiasi ilizama katika Mto Congo karibu na kijiji cha Longola Ekoti, mkoani Mai-Ndombe magharibi mwa nchi, usiku wa kuamkia jana.

Amesema kufikia sasa miili 60 imeopolewa kutoka kwenye maji ya mto huo, na kwamba walionusuriwa kufikia sasa ni watu 300. Waokoaji wanaendelea na kazi ya kutafuta miili na watu waliotoweka katika eneo hilo la magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mbikayi amesema boti hiyo iliyokuwa imebeba watu zaidi ya 700 ilikuwa ikitokea Kinshasa, mji mkuu wa DRC ikielekea mkoa wa Equator kabla ya kutokea ajali hiyo.