Wanafunzi, walimu na jamaa waliokuwa wametekwa nyara wiki mbili zilizopita katika shule moja Kaskazini mwa Nigeria wameachiliwa huru jana Jumamosi. 

Gavana wa jimbo la Niger Abubakar Sani Bello amesema kuwa jana Jumamosi aliwapokea wanafunzi 24, walimu sita na jamaa wengine nane baada ya kuachiwa huru majira ya Asubuhi. 

Hata hivyo idadi hiyo inatofautiana na idadi ya watu waliosemekana kutekwa ambao ni 42, ikiashiria kuwa baadhi yao bado hawajulikani walipo. 

Kuachiwa kwao kumetangazwa siku moja baada ya polisi kusema watu wenye silaha wamewateka wasichana 317 kutoka shule ya bweni katika eneo jingine Kaskazini mwa Nigeria katika jimbo la Zamfara. 

Makundi makubwa ya watu wenye silaha yanaendesha shughuli zake katika jimbo la Zamfara ingawa polisi inasema ni makundi ya majambazi. .