Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limefanikiwa kuwakamata Waethiopia 07 kwa kosa la kuingia nchini bila kufuata taratibu za nchi.

Ni kwamba tarehe 09.02.2021 majira ya saa 14:00 mchana huko kijiji na kata ya Changalawe, Tarafa Kiwanja, wilaya ya Chunya , Mkoa wa Mbeya . Askari Polisi wakiwa doria walikamata Gari yenye namba za usajili T.257 DAY aina TOYOTA NOAH iliyokuwa ikiendeshwa na dereva aitwae CHRISTOPHER S/O MASESE [37] Mkurya, na KHALFAN S/O KHATIBU [34] Msukuma wote Mkazi wa Igoma Mwanza.

Askari walianza kufanya ukaguzi kwenye gari hilo na ndipo walimkamata BDASALO S/O TESEF [27] Raia na Mkazi wa nchini Ethiopia akiwa na wenzake 06 kwa kosa la kuingia nchini bila kibali.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya, tunaendelea na mahojiano dhidi ya watuhumiwa CHRISTOPHER S/O MASESE [37] na KHALFAN S/O KHATIBU [34] madereva  waliokuwa wakisafirisha wahamiaji hao ili kuendelea kubaini mtandao mzima wa mawakala wa kusafirisha wahamiaji.

Mtakumbuka tarehe Januari 13, 2021 huko kijiji cha Gari Jembe Wilaya ya Mbeya Vijijini, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanikiwa kuwakamata waethiopia 61 kwa kosa la kuingia nchini pasipo kibali.

MAUAJI.
Jeshi la polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia AHADI S/O ANGETILE [18] mnyakyusa, mkazi wa kitongoji cha Ibwe, kijiji cha Mpunguti, Kata Lubeta, Tarafa ya Busokelo, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya kwa tuhuma ya mauaji ya mtoto aitwae PROSPER S/O PARADISO [5]  mnyakyusa, mkazi wa Ibwe Kata Lubeta, Tarafa ya Busokelo, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya.

Ni kwamba mnamo tarehe 09.02.2021 majira ya 12:00 mchana huko katika kitongoji cha Ibwe, kijiji cha Mpunguti, Kata Lubeta, Tarafa ya Busokelo, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa

 Mbeya marehemu PROSPER S/O PARADISO, alifariki dunia baada ya kupigwa na mtuhumiwa [AHADI S/O ANGETILE] ambaye ni baba yake mdogo.

Chanzo cha tukio hili ni mtuhumiwa kutukanwa na marehemu ndipo alikasirika na kuanza kumpiga maeneo ya kichwani na tumboni kwa kutumia Fimbo.

Kwa mujibu wa taarifa za wanafamilia inaelezwa kuwa mtuhumiwa ana matatizo ya akili.

WITO WA KAMANDA.
Ninatoa wito kwa wasafirishaji wa wahamiaji haramu nchini kujiepusha  kufanya biashara haramu ya binadamu kwani ni kinyume cha sheria za kimataifa na hata maadili na dini inakatazwa.

Kwamba wanaojihusisha na biashara hiyo wajue kusafirisha wahamiaji haramu ni kosa la Jinai lenye adhabu kali na vyombo vinavyotumika kuwasafirisha hutaifishwa kwa amri za Mahakama.

Ninaendelea kuwakumbusha wananchi kwamba Mbeya hapapenyeki na iwapo utajaribu tu kufanya biashara hiyo haramu utaishia mkononi mwa vyombo vya dola kwani tumejipanga vilivyo kuzuia na kupambana na uhalifu na wahalifu wa kila aina.

Imetolewa na:
[ULRICH O. MATEI -SACP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA.