Maafisa waandamizi katika ikulu ya White House wamesema mswada wa Rais Joe Biden unaolenga kutoa uraia kwa wahamiaji milioni 11 wasio na vibali nchini Marekani, utawasilishwa bungeni kwa ajili ya majadiliano. 

Wabunge wawili wa chama cha Democratic, Linda Sanchez wa jimbo la California na seneta wa New Jersey Bob Mendez watawasilisha mswada huo katika bunge la wawakilishi na seneti. 

Mswada huo unatarajiwa kuwapa uraia wahamiaji hao iwapo wataweza kuthibitisha kwamba walikuwa Marekani kuanzia Januari Mosi 2021. Mswada huo utawanufaisha pia watu watu waliopelekwa Marekani kinyume cha sheria kama watoto na wakakulia nchini humo. 

Rais Barack Obama mwaka 2012 alitoa amri ya kulindwa kwa wahamiaji hao na pia kuruhusiwa kufanya kazi ila mrithi wake Donald Trump alitishia kufutilia mbali mpango huo kama sehemu yake ya kupambana na uhamiaji wa aina yoyote ile.