Na: Mwandishi Wetu – Dodoma
Watu wenye Ulemavu wanaweza kufanya shughuli mbalimbali ambazo zitawawezesha kujikwamua kiuchumi na kujiletea maendeleo bali wasichukulie ulemavu walionao kama ndio hali ya kutokuweza kujishughulisha na masuala mbalimbali ya kijamii, kiuchumi ama kisiasa.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama wakati wa hafla ya ugawaji wa vifaa saidizi kwa Watu wenye Ulemavu ikiwemo Miguu ya bandia iliyotolewa kwa wanufaika 50 ambayo imetolewa na Kampuni ya Kamal Group kupitia programu yao ya Empowering People.
Waziri Mhagama alieleza kuwa serikali hii ya Awamu ya Tano inatambua michango inayotolewa na wadau mbalimbali katika kusaidia watu wenye ulemavu na ni dhairi kuwa tunashuhudia namna uongozi mahiri wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli tangu aingie madakani amekuwa mstari wa mbele katika kutoa kipaumbele kwa wanyonge ikiwa ni pamoja na watu wenye ulemavu.
“Tunamifano dhahiri shahiri kabisa kwamba Rais wetu anawajali Watu wenye ulemavu na tangu alipoingia tu madarakani aliamini watu wenye ulemavu wanauwezo wa kufanya mambo mbalimbali na katika kuamini hayo ameweza kuwateua kwenye nafasi mbalimbali za uongozi, hivyo mtambue kuwa mnauwezo wa kufanya mambo makubwa,” alisema Waziri Mhagama.
Aliongeza kuwa, Ofisi ya Taifa ya Takwimu mwaka 2019 – 2020 ilikadiria watanzania wamefika mil. 55.9 kati yao mil. 2.5 ni Watu wenye Ulemavu ambao wanaulemavu wa aina mbalimbali na wanauhitaji wa mahitaji mbalimbali ikiwemo elimu, miundombinu fikivu, huduma za afya, kuwezeshwa kiuchumi n.k
“Tukio hili la leo la kugawa miguu hii bandia kwa wenzetu wenye ulemavu inaonyesha jinsi gani tunawajali, hivyo ningependa kuona programu hii ya kuwasaidia watu wenye ulemavu vifaa hivi saidizi kupitia kampuni ya Kamal inaendelea kufanyika nchi nzima ili kuwasaidia watu wenye ulemavu kwa zaidi,” alisema Mhagama
“Kampuni hii ya Kamal Group pamoja na Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC Plc.) wamekuwa mfano mzuri wa kuigwa kwa namna mbavyo wamekuwa wakijitolea kwa jamii kwa kutoa huduma mbalimbali ambazo zimejikita katika kuwasaidia wenzetu wenye ulemavu ikiwemo viti mwendo, vioski tembezi ambavyo vimewasaidia watu wenye ulemavu kujiajiri na kuchangia pato la uchumi wa taifa pamoja na kutunza familia zao,” alifafanua Mhagama
Aidha, Waziri Mhagama alitoa wito kwa watu wenye ulemavu kutumia vifaa saidizi hivyo walivyopatiwa kwa kujishughulisha kwenye mambo yenye kuwaletea manufaa badala ya kuvitumia kwenye vitu visivyo na msingi kwao. Pia alitoa wito kwa makampuni mengine binafsi kuendelea kushirikiana na serikali kwa kujitolea na kushiriki kwenye masuala mbalimbali ya kujitolea katika jamii hususani kwenye eneo la faida wanayopata.
Sambamba na hayo, alikemea vitendo vya utumikishwaji wa watu wenye ulemavu kuomba fedha mitaani na kueleza kuwa suala hilo ni kosa la jinai na ni udhalilishaji wa watu wenye ulemavu, hivyo oparesheni ya kuwasaka wanaojishughulisha na masuala hayo inaendelea, mtu yoyote atakayekutwa anajishughulisha na masuala hayo atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Pia, Waziri Mhagama aliwataka watu wenye ulemavu kuchangamkia fursa ya mikopo inayotolewa na halmashauri kupitia mapato ya ndani ili waanzishe shughuli au miradi itakayowainua kiuchumi.
Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Wenye Ulemavu), Mhe. Ummy Nderiananga aliupongeza Uongozi wa Kampuni ya Kamal Group kwa kujitolea kusaidia watu wenye ulemavu kupitia pato walilopata kama kampuni na kuamua kujitolea kwa kundi la watu wenye ulemavu.
“Serikali inawajali watu wenye ulemavu na imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali lengo ikiwa ni kuboresha huduma zaidi kwa kundi la watu wenye ulemavu,”
“Wale watakaopata miguu hii ya bandia mkaitumia fursa hiyo kutoka na kufanya kazi ili mjiletee maendeleo kwa kuwa mnauwezo mkubwa wa kuchangia pato la taifa,” alisema Naibu Waziri Ummy.
Kwa Upande wake, Mbunge wa Dodoma Mjini, Mhe. Anthony Mavunde (Mb) alieleza kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli imekuwa ni serikali inayowajali wanyonge lakini vilevile imeonyesha mwelekeo mzuri wa kuwajali watu wenye ulemavu.
“Viungo hivi vitawasaidia ndugu zetu wenye ulemavu kubadilisha maisha yao kwa kuwa wataweza kufanya shughuli mbalimbali kwa urahisi sambamba na kubadili mifumo ya maisha yao,” alisema Mavunde
Akizungumza kabla, Mwakilishi kutoka Kampuni ya Kamal Group, Bi. Hedwick Pinda alieleza kuwa mwaka huu 2021 kampuni hiyo imejipanga kutoa vifaa saidizi ikiwemo miguu bandia 200 ambayo inatengenezwa hapa hapa nchini katika kiwanda cha Kamal Steel itatolewa kwa wahitaji, sambamba na hayo alieleza pia Kamal Group imekuwa ikitambua vipaji mbalimbali walivyonavyo watu wenye ulemavu na kuwawezesha kujiendeleza.