Na Samirah Yusuph, Simiyu

Simiyu. Kumekuwa na kasumba ya mawakala wanapo fanya usajili wa laini za simu kumtaka mteja kurudia mara kadhaa kuweka alama ya kidole ili kuthibitisha usajili kwa kigezo cha kutanya zoezi hilo kwa usahihi.


Kasumba hiyo imekuwa ni mtaji kwa mawakala ambao baadhi yao hutumia alama hizo kusajili laini za simu zaidi ya moja ili baadae kuziuza kwa watu wenye uhitaji wa laini za simu zilizosajiliwa kwa matumizi binafsi.

Hali inayomfanya mteja mwenye namba ya NIDA kusajili namba ambazo zitatumiwa na watu wengine bila yeye kufahamu jambo hilo.

Akizungumza namna ambavyo amejikuta akipoteza namba yake ya simu Huzaima  alisema kuwa zoezi la uhakiki wa namba za simu lilimfanya kugundua kuwa namba yake ya NIDA imesajili laini za simu Tatu.

Anasema alikwenda kufuta namba kwa wakala mtaani lakini alijikuta wakala anafuta namba yake na kuongeza namba zake nyingine bila yeye kujua, alipokwenda makao makuu ya kampuni ya simu namba yake haikuweza kurudishwa sababu ilifutwa kabisa

Aliongeza kuwa msaada aliopata ni kurudisha kiasi cha fedha kilichokuwa kwenye laini yake ya simu pekee lakini namba ya simu aliipoteza.

Kwa kupiga namba *106# katika simu Mteja ataongozwa kupata uhakiki wa namba yake yake ya simu pamoja na kutazama namba za simu zilizosajiliwa kwa namba yake ya NIDA.

Baada ya kufuata hatua hizo za kutazama namba zilizosajiliwa kwa namba ya NIDA Rose  anasema kuwa alikuta namba kumi na nane ambazo zimesajiliwa kwa namba yake ya NIDA, Nne pekee zikiwa ni za kwake kutoka katika makampuni manne ya simu.
 

Ilibidi kufika katika madawati ya huduma ya wateja katika makampuni yote ili aweze kufuta namba ambazo hakuzitambua, kwa sababu hakufahamu matumizi ya namba hizo kwa watu waliokuwa nazo ilihali taarifa zote za namba ni za kwake


Wakieleza namna ulaghai huo unavyofanyika kwa sharti la kutokutajwa jina baadhi ya mawakala katika soko la mji wa Bariadi walisema kuwa zoezi hilo huanza na namba ya NIDA ya wakala mwenyewe baada ya kuwa amekamilisha kiwango cha usajili kwa namba tano katika kila kampuni la simu ndipo hutumia namba za wateja.

Ili kumfanya mteja asigundue kwa urahisi kuwa namba yake ya NIDA imesajili namba nyingi huanza kwa kuihakiki na kuichagua namba hiyo kuwa namba kuu kisha nyingine zote kuzifanya kuwa namba za ziada.

Akizungumzia ulaghai huo meneja wa Tigo mkoa wa Simiyu Amour Temu alisema kuwa jambo hilo linafanywa na mawakala licha ya kuwa ni kosa kubwa kisheria hivyo katika kudhibiti uharifu huo inawalazimu kufanya ukaguzi wa mara kwa mara ili kuwadhibiti mawakala hao.

"Kwa kukagua usajili wa wateja kila siku inasaidia kuzishuku namba ambazo zimefanana majina ya usajili hivyo ukizibaini inakuwa ni rahisi kumgundua wakala aliyefanya hivyo kisha hatua za kisheria zinachukuliwa dhidi yake,"

Maelezo ambayo yalithibitishwa na kamanda wa polisi mkoa wa Simiyu Richard Abwao kwa kutolea mfano kesi ya makosa ya kimtandao iliyotokea katika wilaya ya Meatu, ambapo jeshi la polisi liliwakamata mawakala baada ya kutumia taarifa zao kusajili laini ya simu kwa mtu ambaye hana taarifa za NIDA.

"Kesi kama hizo zipo nyingi, kwa kushirikiana na makampuni ya simu inakuwa ni rahisi kuwabaini watu wanaofanya ulaghai huo, mfano linapotokea tukio la uharifu kwa kutumia namba ambayo taarifa zake ni za mtu mwingine ufatiliaji wake unakuwa ni mrefu kwa maana kosa linakuwa limetendwa na mtu mwingine"alisema Abwao na kuongeza kuwa;

"Hivyo polisi watamkamata mtu ambaye hahusiki na kosa kwa sababu ya taarifa za ile namba pengine kosa hilo linakwamisha upelelezi kwa sababu aliyekusudiwa kukamatwa anakuwa bado hajapatikana, cha zaidi wakala aliyesajili namba ile ndiye ambaye hukamatwa kujibu tuhuma hizo kwa sababu huhusishwa na uandaaji wa uharifu.

Mamlaka ya mawasiliano Tanzania (TCRA), ilitoa muongozo wa usajili wa laini za simu kwa njia ya alama za vidole (kibiometria) kwa malengo manne ikiwamo kuimarisha na kuendeleza juhudi za kupambana na ulaghai katika miamala na huduma za kielektroniki pamoja na kuhakikisha kuwa watoa huduma wanakuwa na utaratibu unaofanana wa kusajili laini katika njia ya kibiometria.

Katika muongozo huo, sehemu ya sita kuzuia ulaghai kipengere cha pili na cha nne kinaeleza kuwa iwapo matukio ya ulaghai yatabainika watoa huduma za simu za mkononi watajitahidi kushirikiana na kutambua ulaghai huo na kuchukua hatua dhidi ya waharifu waliotenda ulaghai huo.

Pamoja na mtoa huduma ambaye atashindwa kuwabaini waharifu wanaofanya shughuli zozote za ulaghai kuhusiana na usajili wa laini kibiometria atawajibika kumfidia mhanga wa ulaghai kwa hasara atakayopata.

Mwisho.